Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Kadri siku zinavyosonga
mbele inakuwa ni desturi kwa baadhi ya wazazi mijini na hata vijijini kutoa
uhuru usio na mipaka kwa watoto wao kwa kisingizio cha kuwapenda au kutotambua
wajibu wao kama wazazi.
Katika zama hizi za
utandawazi kila mzazi au mlezi anapaswa kuwa makini na mtoto wake katika kila
hatua ya ukuaji ili kumuwezesha mtoto huyo kujitambua na kuishi kwa malengo .
Kwenye jamii yetu tunawaona
baadhi ya wazazi ambao wameshindwa kabisa kuwafundisha watoto wao heshima na
utii ikiwemo kutumia vizuri uhuru walionao kama watoto hasa wanapofikia umri wa
kupevuka.
Wazazi wengi na walezi
hudhani kwamba jukumu lao kuu kwa watoto ni kuwapa chakula, malazi, mavazi na
elimu lakini suala la kuwaongoza kimaadili hawalipi kipaumbele hivyo wanawaacha
watoto wajiongoze wenyewe na hatimaye kuibua matatizo makubwa kwenye jamii.
Si ajabu kwa dunia ya sasa
kumkuta kijana au binti wa umri chini ya miaka 18 ni mwanafunzi lakini anamiliki
vitu vya thamani kama simu na kadhalika bila ya mzazi au mlezi wake kuuliza ama
kufuatilia ili kujua amepataje vitu hivyo.
Baadhi ya wazazi hufikia
hatua ya kuwasifia watoto wao ambao bado ni wanafunzi kuwa ni wajanja wanaweza
kujinunulia mahitaji yao wenyewe hivyo wanawapunguzia mzigo wa kuwahudumia.
Wengine huenda mbali zaidi
kufikia hatua ya kuomba msaada wa mahitaji ya nyumbani kutoka kwa watoto wao
ambao wana uhakika kwamba hawana shughuli yoyote ya kuwaingizia kipato.
Wazazi wengine hawajali muda
wa mtoto kutoka na kurejea nyumbani wala kufuatilia mwenendo wake shuleni kwa
maana ya maendeleo yake kitaaluma na tabia kwa ujumla.
Imefika hatua baadhi ya
wazazi kwenye jamii yetu hasa kina mama wanashirikiana na binti zao ambao ni
wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupanga mipango ya kutafuta wanaume
wa kuwanunulia mahitaji mbalimbali ya nyumbani.
Tabia hiyo ya wazazi
kujisahau na kutotimiza wajibu wao katika malezi ya watoto inachangia kwa
kiwango kikubwa kuzalisha matatizo mengi tunayoyaona sasa kwenye jamii yetu
ikiwemo wizi, kuongezeka kwa vitendo vya kikatili, unyanyasaji wa kijinsia,
UKIMWI na mimba za utotoni.
Tumemsikia Mhe. Rais
Magufuli akisema kwamba hataruhusu mwanafunzi yeyote aliyepata ujauzito kurudi
shuleni kwa sababu ruhusa hiyo itawahamasisha wengine kubeba mimba na kukwamisha
juhudi za Serikali za kutoa elimu bora kwa kila mtanzania.
Ni wajibu wetu sasa wazazi
na walezi kuhakikisha watoto wetu hasa mabinti wanajitambua na kuepuka vishawawishi
vya aina yoyote vitakavyoweza kuwaharibia maisha yao na ndoto zao.
Watoto wa kiume pia
wanapaswa kuangaliwa na kufuatiliwa kwa karibu na tuache kasumba ya kudhani
kwamba watoto wa kiume hawahitaji uangalizi kwani na wao wanapata athari kama
watoto wa kike.
Kila mzazi au mlezi atambue
kuwa suala la maadili ya mtoto ni jukumu lake la msingi katika kuhakikisha
ustawi wa mtoto huyo kwenye elimu, afya, na makuzi kwa ujumla.
Kaulimbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu ni “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto” Kaulimbiu hii inawataka wazazi, walezi, Serikali na
wadau wengine kutimiza wajibu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo
ya mtoto ili iweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili
nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.
0 comments:
Post a Comment