KATIKA kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, Wilaya ya
Mpwapwa mkoani Dodoma imeweza kuteketeza ekari 10 za mashamba ya bangi
huku watuhumiwa 34 walipatikana na dawa za kulevya aina ya bangi
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri, wilaya
hiyo ni miongoni mwa wilaya zilizo katika mapambano ya dawa za kulevya,
ambapo katika kipindi cha Januari hadi Juni 2017, wilaya hiyo iliweza
kuteketeza mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 10 katika maeneo
matatu tofauti.
Pia alisema kwa nyakati tofauti, jumla ya watuhumiwa 34 walikamatwa
baada ya kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi. Alisema kati ya
watuhumiwa waliokamatwa, 16 walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo kati
ya mwaka moja hadi miaka 30 pamoja na kulipa faini.
Pia alisema bangi iliyokamatwa ni gunia moja, kilo moja na gramu 542,
misokoto tisa na kete 121. Shekimweri alisema wilaya inaendelea kutoa
elimu kwa vijana wasijiingize katika matumizi ya dawa za kulevya ambapo
pia wilaya imeanzisha kikundi cha vijana cha waliokuwa wanatumia dawa
hizo ili waweze kuwaelimisha wenzao madhara ya dawa hizo na kuziepuka.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment