Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Mawasiliano), Dkt. Maria Sasabo,(kushoto) amezungumzia umuhimu wa taasisi za umma zilizo
chini ya mradi wa Benki ya Dunia kuhakikisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA), iliyofungwa inafanyakazi mara moja ili kuongeza tija na
ufanisi katika kuhudumia wananchi.
Akizungumza wakati wa
ziara yake ya kukagua ufanisi wa matumizi ya TEHAMA katika hospitali ya rufaa
ya Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Dkt. Sasabo amewataka viongozi wa taasisi hizo kuhakikisha
mifumo hiyo inakamilika na kuanza kazi mara moja.
“Hakikisheni ifikapo
mwezi Septemba mawasiliano yenu na huduma zenu zilizounganishwa kwenye mifumo
ya TEHAMA inafanyakazi ili kurahisisha utendaji na kuiongezea Serikali mapato”,
amesema Dkt. Sasabo.
Dkt. Sasabo amemtaka Kaimu
Mganga Mkuu wa hospitali ya rufaa ya Dodoma Dkt. Samweli Seseja, kuhakikisha
hospitali hiyo inakuwa na mfumo maalum wa mawasiliano utakaowezesha kuboresha
huduma katika hospitali hiyo na kumudu ongezeko la watu katika Manispaa ya
Dodoma.
Akiwa wilayani Bahi,
Katibu Mkuu huyo wa mawasiliano amemtaka
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bahi
Bi, Rachel Chuwa kuhakikisha mifumo ya Tehama iliyofungwa katika ofisi za halmashauri hiyo na katika
shule za sekondari wilayani humo inafanyakazi mara moja ili kuendana na malengo
ya serikali katika utoaji wa huduma bora, za kisasa na kwa wakati kwa wananchi
wake na hivyo kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa
kati ifikapo mwaka 2025.
Serikali imekuwa
ikihamasisha matumizi ya TEHAMA katika taasisi zake zikiwemo ofisi, shule, hospitali
na vituo vya polisi ili kuboresha huduma
na kuwezesha uwazi katika ukusanyaji wa mapato na hivyo kuhamasisha wananchi
kuchangia huduma kwa hiari.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na
Mawasiliano.
0 comments:
Post a Comment