Naibu
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Mheshimiwa Suleiman Jafo akimkabidhi mshindi wa tatu wa maonyesho ya
nanenane kanda ya kati ambaye ni Jeshi la Magereza.
Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman Jafo akimkabidhi mshindi wa pili wa
maonyesho ya nanenane kanda ya kati ambaye ni Benki Kuu ya Tanzania
Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman Jafo amezitaka
halmashauri zote nchini kutekeleza jukumu lao la kuwapelekea wakulima wa
vijijini teknolojia na pembejeo bora ili kuongeza tija katika shughuli
za uzalishaji mali.
Jafo
ametoa rai hiyo jana wakati wa kilele cha maonyesho ya nanenane kanda
ya kati inayojumuisha mikoa ya Singida na
Dodoma ambapo alipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali
yalioonyesha shughuli za kilimo na ufugaji pamoja na sekta binafsi
zinazosaidia katika kukuza uchumi.
Amesema kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ni “Zalisha
kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati”
hivyo basi halmashauri zinatakiwa kuhakikisha mazao ya wakulima na
wafugaji yanapata
soko kwa kutoa elimu ya kuchakata na kufungasha bidhaa zao katika ubora
unaokubalika sokoni ili mazao hayo yawe na thamani zaidi.
Jafo
amesema halmashauri zote zinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa kutenga
maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na
kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa na huduma zote za msingi kama vile
miundombinu ya Barabara, Umeme na Maji ili kuwavutia wawekezaji na hivyo
kumsaidia mkulima na mfugaji kufikia uchumi wa kati.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Ole Nasha ameipongeza Benki ya Maendeleo
ya Kilimo kwa kuendelea kuwezesha shughuli za kilimo nchini huku akitoa angalizo la kutowasahau wakulima wasio na uwezo.
Ole Nasha amesema Benki hiyo isitoe mikopo kwa wakulima wakubwa na wenye uwezo tu bali isisahau jukumu la kuwafikia
wakulima wasio na uwezo ili waweze kupata mikopo na kuweza kulima kisasa kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Wakati huo huo Naibu waziri Jafo ametoa Wito kwa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kuamua kuufanya Mkoa wa Dodoma hasa
Viwanja vya Nzuguni kuwa Kituo cha Kudumu cha Maonesho ya nanenane kitaifa kutokana
na Kijiografia
kuwa katikati na Makao Makuu ya nchi na hivyo kuwa rahisi kwa Kanda
zote nchini na hata nchi za jirani kuja kushiriki Maonesho ya Nane Nane.
Jafo amesema hayo akiunga mkono kauli iliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba
aliyesema Serikali inafikiria kuachana na utaratibu wa kuhamisha hamisha
Maonesho
ya kitaifa ya Nane Nane kwenye Kanda mbalimbali na badala yake kuwa na
kituo kimoja cha Kitaifa kama ilivyo kwa maonesho ya Kimataifa ya
Biashara (Sabasaba) yanavyofanyika Dar es Salaam pekee.
Jafo
amesema Uwanja wa Nane Nane Nzuguni unahitaji kufanyiwa uwekezaji na
uendelezaji wa miundombinu yake kama barabara,
umeme na maji na kuboreshwa huduma mbalimbali na kuzitaka Mamlaka za
Serikali za Mikoa ya Dodoma na Singida kuweka mkakati wa kuendeleza
miundombinu hiyo kwa kuwa baada ya uwekezaji mkubwa uwanja huo
utarejesha mapato mengi.
Ameongeza kuwa Serikali za Mikoa ya Singida na Dodoma inaweza kufanikisha ukarabati huo kwa kushirikisha wadau mbalimbali
wakiwemo Taasisi kama Benki ya Uwekezaji TIB na Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB.
Washindi
wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati yaliyoanza tangu Agosti Mosi ni
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lililoibuka
kuwa Mshindi wa jumla wa Maonesho ya Mwaka huu, likifuatiwa na Benki Kuu
ya Tanzania ikiwa mshindi wa pili na Mshindi wa tatu akiwa ni Jeshi la
Magereza.
0 comments:
Post a Comment