Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
IDARA ya Uhamiaji imekiri kuwapo upotevu wa mapato kwenye kitengo cha
utoaji viza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA), Dar es Salaam.
Imesema ili kukabiliana na hali hiyo pamoja na mambo mengine
imeanzisha huduma za kimtandao.
Aidha, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wametuhumu idara katika
uwanja huo wa ndege kugubikwa na rushwa jambo ambalo limekuwa
likisababisha usumbufu kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini kwa
kuwacheleweshea au kuwazungusha kupata huduma.
Hayo yalibainishwa jana kwenye kikao cha PAC na watendaji wa idara
hiyo wakiongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Projest Rwegasira, waliokiri kuwapo upotevu wa mapato yatokanayo na
malipo ya viza ambao tayari umetafutiwa utatuzi. “Kwenye suala la viza
ni kweli fedha nyingi zimekuwa zikipotea,” alisema Kamishna wa Utawala
na Fedha, Edward Chogero na kufafanua kuwa pamoja na hatua nyingine,
wako kwenye mchakato wa kuanzisha mfumo wa viza mtandao.
Alikiri tatizo hilo na kusema wameanza mchakato wa kuhakikisha fedha
hazipotei na pia wanadhibiti rushwa. Alisema ipo timu inayoundwa na
wadau wote wakiwemo Wizara ya Fedha na Mipango, Uhamiaji, Usalama wa
Taifa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ajili ya
kuboresha viza mtandao ili fedha ziwe zinaingia moja kwa moja serikali
badala ya kuingia mikononi mwa watu .
Chogero alisema baada ya kuona mianya ya rushwa ikiwamo foleni katika
JNIA, wameongeza madirisha ya malipo yawe 10 kiasi ambacho hakuna
mtumishi anayeweza kuomba rushwa ili amhudumie mteja haraka. Kwa upande
wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege Kilimanjaro (KIA), alisema kulikuwa na
kompyuta tatu na wiki iliyopita wameongeza zimefika tisa.
“ Tunajaribu kuimarisha na tumepata fedha kutoka serikali, wakati
tunaendelea kuimarisha mfumo, tutapata fedha kwa ajili ya vituo vilivyo
mkoani.
Hakuna mtu atagongewa muhuri tu bila kuwekewa stika,” alisema.
Awali, katika hoja za wajumbe wa kamati kuhusu upotevu wa mapato, Mbunge
wa Magomeni, Jamal Kassim (CCM) akinukuu taarifa ya ukaguzi ya CAG
mwaka wa fedha 2015/2016 , alisema sampuli ya wageni 65 iliyochukuliwa
JNIA, baada ya kufuatilia ilibainika kati yao, watu 20 taarifa zao za
malipo ya viza hazikuwapo.
Akizungumzia rushwa, Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe (CCM)
alisema JNIA umechafuka kwa vitendo hivyo vinavyofanywa kwa nguvu na
baadhi ya watumishi dhidi ya wageni na kuwakatisha tamaa.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, mgeni anaweza kuzungushwa au kuwekewa
vikwazo katika kupatiwa huduma ili atoe rushwa. Alitoa mfano kuwa yupo
jirani yake, ana mdogo yake anayechezea timu ya Simba, alipata wageni
kutoka Ivory Coast ambao baada ya kufika, walitaka watokee nchini kwenda
Vietnam, lakini waliwekewa vikwazo kwamba lazima warudi nchini kwao
ndipo waende nchi hiyo.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment