Imeandikwa na Mwandishi Maalum, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka mawaziri na naibu mawaziri
wajiepushe na utoaji wa matamko yasiyotekelezeka ili kuepuka
mikanganyiko serikalini.
Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akifungua kikao kazi cha mawaziri
kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina mjini Dodoma. Alisema ni vema
viongozi hao kabla ya kutoa matamko wakajiridhisha iwapo jambo hilo
halitaleta athari za kibajeti na kisera na kama lipo katika bajeti za
wizara zao.
Pia aliwataka viongozi hao wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya
uongozi ili kuithibitishia jamii kuwa Rais John Magufuli aliwateua
kutokana na uadilifu na uwezo wao kiutendaji. “Tunao wajibu mkubwa
kuhakikisha kwamba kila mmoja wetu anafanya kazi kwa nguvu na bidii ili
kutimiza matarajio ya Rais Magufuli na wananchi wote kwa ujumla,”
alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wajiwekee utaratibu wa
kusikiliza hoja na shida za wabunge na kuchukua hatua kwa mujibu wa
sheria, taratibu na kanuni. Pia amewataka wafanye ufuatiliaji na
tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu
sekta zao kwa kuwa wao ni wasimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya
serikali.
Waziri Mkuu alisema mawaziri na naibu mawaziri wanatakiwa wasimamie
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2016/2017 hadi
2020/2021. Pia wasimamie utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais
Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment