VYOMBO vya dola vimeagizwa kumchunguza Waziri wa zamani wa Maliasili
na Utalii, Lazaro Nyalandu akidaiwa kuitia hasara Serikali. Vyombo
hivyo, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na Jeshi la
Polisi, vimetakiwa kumchunguza kutokana na kushirikiana na Kampuni za
Uwindaji na kuwapa vitalu vingi kinyume cha utaratibu.
Uamuzi huo ulitolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi
Kigwangalla wakati akichangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa
Taifa kwa mwaka 2018/19 na mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti
kwa mwaka 2018/19.
Alisema katika miaka miwili akiwa Waziri Nyalandu aliitia hasara
Serikali kwa kutokusanya tozo katika hoteli kubwa nchini za Sh bilioni
32 sawa na Sh bilioni 16 kila mwaka. Alisema mwaka 2014 na 2015,
Nyarandu aliisababishia hasara ya kiwango hicho kwa kutotoza tozo katika
hoteli mbalimbali nchini.
Dk Kigwangalla alisema watu wanasema anafukua makaburi, lakini ili
kufanya kazi vizuri lazima aondoe mitandao ya ujangili iliyokuwepo
wizarani kwanza ndiyo afanye kazi. “Katika miaka miwili 2014-15,
hakusaini Gazeti la Serikali (GN) kwa ajili ya kukusanya kodi kwenye
hoteli mbalimbali nchini kitendo ambacho kimeitia hasara Serikali,”
alisema.
Alisema katika kuonesha ukubwa wa tatizo, hata wapinzani hasa, Mbunge
wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) alilalamika kama Dk
Wilbrod Slaa angepita kuwa rais na Nassari akateuliwa Waziri wa Mambo ya
Ndani, angeshughulika kumwondoa Waziri Nyalandu kutokana na utendaji
mbovu.
Alisema Nyalandu alikuwa anatumia muda mwingi kustarehe na kusafiri
nje ya nchi hasa Marekani na kuishi kwenye hoteli za kimataifa. Dk
Kigwangalla alisema Nassari alikuwa sahihi, kwani Nyalandu alikuwa
akiishi hoteli ya Serena ambayo ni kati ya hoteli ambazo hakusaini GN
yake ilipe tozo au kodi ya hoteli.
Dk Kigwangallah alilieleza Bunge kuwa Nyalandu alikuwa akifanya
starehe katika hoteli ya Serena na kusafiri kwa kutumia helikopta ya
tajiri, bilionea na mwindaji maarufu wa Marekani katika kampeni za urais
mwaka 2015.
Pia alieleza Nyalandu alitoa vibali vya kuwinda katika vitalu vitano
kinyume cha sheria na utaratibu wa ugawaji vitalu kwa kampuni ya Mwiba
Holdings, Tanzania Game Tracking mali ya tajiri mwenye asili ya
Marekani, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria na utaratibu. Dk
Kigwangalla alizidi kulieleza Bunge kuwa tajiri huyo aliendelea kuwinda
licha ya muda kwisha na aliwahi kukutwa na nyara za taifa.
Alisema zama zinabadilika hivyo wakati sasa Nyalandu anatakiwa
kuchunguzwa na akibainika kuitia hasara Serikali anatakiwa kuchukuliwa
hatua za kisheria kwa alichokifanya. Alisema vitalu vya uwindaji
hutolewa Julai hadi Oktoba na kuhoji inakuwaje bilionea wa Kimarekani
aliwinda baada ya muda huo kuisha.
Pamoja na kung’oa mtandao wa ujangili wizarani, Dk Kigwangalla
alisema bado anaweka mkakati wa kuongeza utalii, vivutio vingine na
kuongeza uwekezaji hasa ukanda wa Kusini ambao Serikali imetoa Sh
bilioni zaidi ya 300 kwa ajili ya kuimarisha utalii huo.
Mbali ya Nyalandu, mawaziri wengine waliowahi kuongoza wizara hiyo ni
Arcado Ntagazwa (1988- 1990), Abubakar Mgumia (1990-1993), Juma Hamad
Juma (1999). Wengine ni Juma Ngasongwa (1995-97), Zakhia Meghji
(1997-2005), Anthony Diallo (2005-2007), Profesa Jumanne Maghembe
(2007-08). Wengine ni Mhandisi Shamsa Mwangunga (2008- 2010), Ezekiel
Maige (2010- 2012) Dk Hamisi Kagasheki (2012), Profesa Maghembe
(2016-2017) na sasa Dk Kigwangalla (2017).
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment