Rais
John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Tunduru, Abdallah Mussa kwa kushindwa kumudu majukumu yake.
Kuenguliwa
kwa Mussa kunafanya idadi ya wakurugenzi watendaji wa halmashauri za
wilaya walioondolewa madarakani kufikia watatu ndani ya siku tatu.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mkuu wa kitengo cha mawasiliano
serikalini katika ofisi ya Tamisemi, Rebecca Kwandu imemkariri Katibu
Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Mussa Iyombe akisema jana mjini Dodoma
kwamba kutokana na hatua hiyo, uteuzi wa mkurugenzi mwingine kujaza
nafasi hiyo utafanyika baadaye.
Jumatatu
wiki hii, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa mkurugenzi wa Halmashauri
ya Manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale na wa Halmashauri ya Bukoba,
Mwamtumu Dau baada ya kushindwa kutaja kiasi cha fedha za Mfuko wa
Barabara walizopokea walipoulizwa na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa
Uwanja wa Ndege wa Bukoba.
Taarifa
ya Tamisemi haijaeleza kosa la Mussa zaidi ya kusema ameshindwa kumudu
majukumu yake, lakini mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera alisema
hivi karibuni kuwa ataiandikia ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo, akisema kuna
ufisadi.
Homera
alisema amebaini kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa mabilioni ya fedha za
miradi ya Serikali na kusababisha kutofanya kazi, akitoa mfano
uchakachuaji wa zaidi ya Sh3 bilioni za ujenzi wa miradi ya umwagiliaji.
0 comments:
Post a Comment