Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu
Waziri wa Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye (mwenye koti)
akifuatilia majadiliano baada ya kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Wakala
wa Meli wa Taifa mbele ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu
kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini
Dodoma. Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Prof. Norman Sigalla King
(katikati) akichangia maoni yake kuhusu Muswada huo. Wa kwanza Kulia ni
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Selemani Kakoso.
Mjumbe
wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania Mzee Renatus Mkinga
(aliyesimama) akitoa maoni yake mbele ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya
Miundombinu kuhusu Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa kwenye
kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye (mwenye koti)
akifuatilia majadiliano hayo na wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Kamati
hiyo Mhe. Prof. Norman Sigalla King.
Mjumbe
wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Rukia Kassim
akichangia maoni yake kuhusu Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa
Taifa mbele ya Kamati hiyo na wadau wa sekta ndogo ya usafiri wa majini
kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini
Dodoma.
……………..
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano imewasilisha Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania
mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwenye kikao
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma.
Muswada
huo umewasilishwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye kwa niaba
ya Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Prof. Makame Mbarawa. Wakati akiwasilisha
Muswada huo, Mhandisi Nditiye alisema kuwa Muswada huu unapendekeza
kutungwa kwa Sheria itakayoanzisha Shirika la Uwakala wa Meli ambalo
pamoja na majukumu mengine litakuwa na jukumu la kutoa huduma ya uwakala
wa meli na kudhibiti huduma za usafiri na usalama wa vyombo vya majini.
Ameongeza
kuwa, Muswada huu utaweka mfumo madhubuti wa uendeshaji wa biashara ya
uwakala wa meli na udhibiti wa huduma za usalama wa usafiri wa meli
hivyo utaimarisha udhibiti wa sekta ndogo ya usafiri wa meli na kuifanya
sekta hii kuchangia vyema katika uchumi na kuongeza pato la Taifa.
Muswada huu ni moja ya jitihada za Serikali za kuhakikisha kuwa taasisi
zake zinajiendesha kwa faida, kibiashara, kwa ushindani na kutoa gawio
kwa Serikali ili iweze kuhudumia wananchi kwa kujenga miundombinu ya
kisasa na kuwapatia wananchi huduma mbali mbali za kijamii.
Mhandishi
Nditiye aliyataja majukumu ya Shirika kuwa ni pamoja na uhakiki wa
shehena inayoingia na kutoka kupitia bandari za Tanzania, uondoshaji
shehena za madini, makinikia, wanyama hai, nyara za Serikali, na bidhaa
zinazotokana na madini na udhibiti wa watoa huduma katika sekta ndogo ya
usafiri majini, usalama wa meli na mazingira ya bahari.
Muswada
huu utaipa mamlaka Shirika ya kutekeleza Sheria ya Bahari ya Mwaka
2003, kufanya ukaguzi wa meli za kigeni na udhibiti wa meli
zilizosajiliwa Tanzania, udhibiti wa vivuko vya kibiashara, kuratibu
shughuli za utafutaji na uokoaji, kudhibiti, kuratibu na kulinda
mazingira ya bahari, kuainisha utaratibu wa kutoa na kuhuisha leseni na
udhibiti wa ada na tozo. Pia, Muswada huu unaainisha taratibu na sifa za
kampuni binafsi inayostahili kupewa leseni ya uwakala wa meli.
Katika
hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu
Mhe. Prof. Norman Sigalla King aliwakaribisha wadau wa sekta hii ndogo
ya usafiri wa meli ili waweze kutoa maoni yao kuhusu Muswada huo. Rais
wa Chama cha Uondoshaji na Usafirishaji wa Shehena Tanzania (Tanzania
Freight Forwarders Association) Bwana Stephen J. Ngatunga kwa niaba ya
Umoja huo alisema kuwa wanaiomba Serikali kutenganisha majukumu ya
Shirika linalotaka kuanzishwa kupitia Muswada huu kwa kulipa majukumu ya
kufanya biashara na kuwa mdhibiti wa sekta ili kuepusha mgongano wa
kimaslahi.
Amefafanua
kuwa ni vema kwa Serikali kuanzisha Shirika na kuwa na chombo kingine
cha kudhibiti sekta hii. Wadau wengine waliotoa maoni yao kuhusu Muswada
huu ni pamoja na Chama cha Wanasheria wa Usafirishaji Majini (Maritime
Law Association), Baraza la Watumiaji wa Huduma za SUMATRA
(SUMATRA-CCC), Mawakala wa Wamiliki wa Meli Tanzania (Tanzania Shipping
Agency Association), Taasisi ya Sekta Binafsi (Tanzania Private Sector
Foundation), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Chama cha Wadau wa
Usafirishaji Majini Tanzania (Maritime Association of Tanzania).
Aidha,
Mhandishi Nditiye amewatoa hofu wadau wa sekta hii na kusema kuwa
Serikali imepokea maoni yao na imewataka wadau wafahamu kuwa Serikali
haina nia mbaya na wao, inataka kuwe na maslahi mapana na katika miaka
iliyopita Serikali imepoteza mapato yake katika Sekta hiii. Dhamira ya
Serikali ni kuwa na Shirika litakalodhibiti na kusimamia sekta hii kwa
kuwa Serikali inafahamu kuwa wadau wametoa ajira kwa watanzania hivyo
Shirika litafanya kazi kwa uwazi kabisa.
Alisema
kuwa Muswada huu utaainisha utaratibu wa kuhamisha watumishi kutoka
Idara zinazosimamia usafiri wa majini kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri
wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na kuwapeleka kwenye Shirika
litakaloanzishwa kupitia mapendekezo ya Muswada huu.
Kikao
baina ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu kuhusu
Muswada huo kitaendelea kesho ambapo Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano itahitimisha hoja yake kwa kujibu maoni ya
Kamati na wadau kuhusu Muswada husika.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 comments:
Post a Comment