TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
ENDELEENI KUWAHAMASISHA WANANCHI WAEPUKE TABIA ZEMBE - MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Afya iendelee kuwahamasisha wananchi wabadili mitindo ya maisha ili kuepuka tabia zembe zinazochochea ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa.
“Wizara ya Afya iendelee kushirikiana na wadau kuhamasisha Watanzania kubadili mwenendo wa maisha kwa kuepuka tabia zembe zinazochochea ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa. Tuendelee kuzingatia mazoezi ili kuimarisha afya zetu na kuipunguzia Serikali mzigo wa kugharamia tiba ya magonjwa yasiyoambukizwa,” amesema.
Akizungumza na viongozi, wananchi na wadau mbalimbali walioshiriki mbio za NBC Dodoma Marathon za mwaka 2024 kabla ya kutoa tuzo na zawadi kwenye uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, leo (Jumapili, Julai 28, 2024), Waziri Mkuu amesema takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa idadi ya watu wenye magonjwa yasiyoambukiza imeongezeka.
Amesema magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanaongoza nchini ni pamoja na kisukari, moyo, figo na afya ya akili na akatumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi walioshiriki mbio za hisani za NBC Dodoma Marathon za mwaka 2024. “Kujitokeza kwenu kwa wingi leo, maana yake ni kwamba mmetambua kuwa kukaa bwete ni kukaribisha magonjwa yasiyoambukiza,” amesisitiza.
Waziri Mkuu pia ameitaka Benki ya NBC iendelee kuweka mikakati ya kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa endelevu na yanaendelea kugusa maisha ya Watanzania wengi zaidi.
Vilevile, amezitaka taasisi na asasi zisizo za Serikali zijitokeze kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuandaa matukio kama hayo ili wananchi waanze kuzoea kufanya mazoezi. “Tulishatoa maelekezo kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili wawakusanye wananchi na kufanya mazoezi kama hivi,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha ustawi na afya ya mtoto zikiwemo kutekeleza Mpango wa Mama Samia Mentorship ambao ni mahsusi kwa utoaji mafunzo ya muda mfupi kazini kwa madaktari bingwa na wakunga. “Hadi kufikia Juni 2024, halmashauri 184 zilishafikiwa na mpango huo na idadi ya wanufaika ni watumishi 4,796,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma alisema benki ya NBC ni wadau wakubwa katika sekta ya michezo kwa kudhamini ligi ya soka ya Tanzania yaani NBC Premier League, kamati ya hamasa inayochangia timu za Taifa na pia ni wadau wakubwa katika mfuko wa utamaduni wenye lengo la kukopesha miradi ya kazi za sanaa nchini. Pia wanaendesha marathon ambayo fedha zake hutumika kuchangia huduma za afya.
Amesema kuwa mbali na mbio hizo kutumika kuimarisha afya na kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza, pia zinatumika kama sehemu ya kuibua vipaji kwa wanamichezo hasa wanariadha ambao wamekuwa wakitumika katika michezo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Mapema, akitoa taarifa kuhusu mbio hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema hii ni mara ya tano kwa mbio hizo kufanyika Dodoma huku lengo likiwa ni kutangaza utalii wa Dodoma.
Alisema kwa mara ya kwanza mbio hizo zilifanyika Novemba 11, 2020 zikiwa na washiriki 1,944 na waliweza kukusanya sh. milioni 100 lakini mwaka huu zimeweza kupata washiriki 8,000 ambapo wameweza kukusanya sh. milioni 300.
Amesema makusanyo ya mwaka huu yatatumika kwenye ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa taaluma ya ukunga kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa; pia watasaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ambayo itakabidhiwa kwa taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
“Pia fedha nyingine itatumika kuchangia ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema.
Washiriki wa mbio hizo walikuwa ni wa km.5, km.10, km.21 na km.42
0 comments:
Post a Comment