Home » » Washauriwa kulima mahindi, mbaazi

Washauriwa kulima mahindi, mbaazi


Hamida Shariff, Gairo
WAKULIMA wa mahindi hapa nchini,  wametakiwa kulima kilimo cha mseto kwa kuchanganya zao hilo na zao la mbaazi ambalo uzalishaji wake sasa umefikia tani tano kwa hekta moja, kwa mujibu wa taarifa za utafiti.
                                                                                                                                                            Taarifa za utafiti huo zilielezwa juzi katika maadhimisho ya siku ya wakulima ya kuonesha kilimo cha mseto cha mahindi na mbaazi, yaliyofanyika katika Kijiji cha Kiyegea, wilayani Gairo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo,Meneja Mradi wa Mageuzi ya Kilimo Nchini (AGRA),Stephen Lyimo, alisema ongezeko la uzalishaji huo linatokana na zao la mbaazi kuchanganywa na mahindi.

Alisema zao hilo limekuwa likiongeza kirutubisho cha Naitrojeni ardhini kwa kutumia mbolea za minjingu chengachenga na virutubisho vingine.
Meneja huyo ambaye pia ni mtafiti kutoka katika Kituo cha Selian, alisema kilimo hicho cha mahindi na mbaazi kinachangia kuwepo kwa uhakika na usalama wa chakula katika kaya.

“Kilimo hicho cha mahindi na mbaazi kinaongeza kipato na hatimaye kuboresha maisha ya mkulima wanaotumia teknolojia hiyo,” alisema.

Mratibu wa mradi huo katika Kanda ya Mashariki, Meshack Makenge, kutoka Kituo cha Utafiti cha Ilonga, alisema mafanikio hayo yanatokana na vituo vya utafiti kuboresha mbegu za mbaazi kulingana na sehemu husika.

Alizitaja mbegu hizo kuwa  ni pamoja na    Komboa inayostawi ndani ya muda wa miezi minne,Tumia inayotumia miezi sita na Mali inayotumia miezi saba.

Mmoja wa wakulima wa zao hilo katika Kijiji cha Lubeho, wilayani Gairo, Stefano Mgweno alisema amekuwa akilima ekari 20 kila mwaka.

Alisema kuwa kutokana na zao hilo ameweza kupata mafanikio ikiwa ni pamoja na kununua mashine ya kusaga, ng’ombe wa maziwa na kusomesha watoto wake .
Chanzo: Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa