Home » » Ualimu mwakani ni pointi 26

Ualimu mwakani ni pointi 26


na Happiness Mtweve, Dodoma
SERIKALI imesema imeweka kiwango cha pointi 27 watu waliomaliza kidato cha nne na kutaka kujiunga na vyuo vya ualimu, lengo likiwa ni kuboresha sekta ya elimu nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Naibu Waziri wa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo wakati alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Manyovu (CCM) Albert Ntabaliba aliyetaka kujua kwa nini wizara hiyo imeweka kigezo cha pointi 27 katika vyuo vya ualimu licha ya baadhi ya vijana 78,000 wa Kasulu wenye pointi 28 tayari walishatuma maombi yao.
Mbunge huyo alitaka kujua Wizara hiyo ilipanga walimu kwa kuzingatia mahitaji ya walimu na inatoa kauli gani kwa wale ambao wana pointi 27 wakati kuna uhaba wa walimu?
Akijibu swali hilo Mulugo alisema Mwaka jana jumla ya vijana 78,000 waliomba nafasi ya kujiunga na ualimu, lakini Wizara hiyo ilikuwa inahitaji jumla ya vijana 7000 na Mwaka huu ni mahitaji ya walimu 6800.
“Lengo hapa ni kuweza kuboresha Sekta hii ya Elimu na kwa mwaka ujao tunaweza kuhitaji Walimu wenye pointi 26 ili tuweze kuwa na elimu yenye ubora wa hali ya juu,” alisistiza Mulugo.
Aidha alisema asilimia 54 ya Walimu ambao walipangiwa katika Wilaya ya Kasulu hawakuripoti ila baada ya Wizara hiyo kutoa agizo la kuwataka walimu hao waripoti kwani iliwaambia wasipofanya hivyo wangelifukuzwa kazi na hivyo walimu hao waliripoti mara moja.
Katika swali la Msingi la Mbunge huyo ambalo lilikuwa na vipengele viwili ambapo kipengele (a) alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka walimu wakutosha katika Vijiji vya Wilaya Mpya ya Buhigwe? Wakati kipengele (b) kilikuwa kinauliza kama Serikali itakubali zitengwe nafasi katika Vyuo vya Ualimu vya Kabanga na Kasulu ili kupunguza tatizo hilo la walimu.
Akijibu Swali hilo Naibu Waziri huyo alisema ni kweli kuna upungufu wa Walimu katika baadhi ya shule hapa nchini zikiwemo shule za Wilaya mpya ya Buhigwe na kwamba katika mwaka wa fedha 2011/2012 Wilaya ya Kasulu ilipangiwa walimu wa cheti 222, stashahada 73 na shahada 94.
Mulugo alisema kwa kuwa wakati huo Buhigwe ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Kasulu ilipata mgawo wake kupitia Wilaya hiyo na katika mwaka huu wa fedha Wilaya mpya ya Buhigwe zitapewa mgawo wa Walimu waliohitimu kupitia Halmashauri husika.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa