Home » » Waziri Maghembe atangaza neema ya maji nchini

Waziri Maghembe atangaza neema ya maji nchini


Na Maregesi Paul, Dodoma
SERIKALI imetangaza neema ya kukabiliana na uhaba wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na makao makuu ya mikoa nchini.
Kauli hiyo, ilitangazwa jana bungeni mjini hapa na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa Fedha 2012/13, ambapo alisema utekelezaji wa mpango wa dharura utasaidia kuondoa hali hiyo.

Alisema yupo katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na miji ya Kibaha na Bagamoyo. 

Alisema mpango huo, unalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 300,000 kwa siku kwa sasa hadi mita za ujazo 710,000 kwa siku ifikapo mwaka 2014. 

Waziri huyo wa maji, alisema Serikali inatekeleza Mpango huo kwa kushirikiana na Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC), Serikali ya Norway, Serikali ya India na washirika wengine wa maendeleo kupitia Mfuko wa Pamoja wa Maji.

Akizungumzia upanuzi wa mradi wa maji wa Ruvu Juu, alisema Mhandisi Mshauri, ameshaanza kazi ya usanifu wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu na bomba kuu la maji linalotoka Mlandizi Pwani hadi Kimara, Dar es Salaam, tangu Machi, mwaka huu.

Alisema upanuzi wa mradi huo, utasaidia kuongeza uwezo wa mtambo kutoka mita za ujazo 82,000 kwa siku hadi mita za ujazo 196,000 kwa siku, ili kukabiliana na ukuaji wa miji ya Mlandizi, Kibaha na Dar es Salaam.

Alisema chini ya utekelezaji wa mpango huo, Serikali itaimarisha miundombinu, inakabiliana na ongezeko la watu na pia inahakikisha maji yanapatikana kwa wingi, ikiwamo wakati wa kiangazi ambapo maji ya Mto Ruvu hupungua.

Kuhusu mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Kahama, Shinyanga, alisema Serikali imeendelea kuusimamia ambapo upatikanaji wa maji katika mji wa Shinyanga na Kahama, umeongezeka.

Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, upatikanaji wa maji katika mji wa Shinyanga, umeongezeka kwa kuwa wanaopata maji ni wateja 13,827, ikilinganishwa na wateja 13,117 waliokuwa wakipata maji Machi, mwaka huu.

Kwa upande wa mji wa Kahama, alisema wanaopata maji ni wateja 8,856 waliokuwa wakipata huduma hiyo Machi, mwaka huu, ikilinganishwa na wateja 8,308, waliokuwa wakipata maji mwaka jana.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa