na Hamida Ramadhani, Dodoma
IMEELEZWA kuwa tatizo kubwa linalowakabili vijana na taifa katika suala zima la ukosefu wa ajira nchini ni kutokana na wengi wao kuwa na tabia ya kuchagua kazi za kufanya.
Hayo yalisemwa jana na Mbunge wa Viti Maalumu wa (CHADEMA) Cecilia Paresso kwenye mdahalo wa kujadili tatizo la ajira kwa vijana ulioandaliwa na Taasisi ya Tuzo ya kitaaluma Tanzania(TAAA).
Paresso alisema kuwa tatizo la ukosaji ajira kwa vijana nchini limekuwa ni sugu kutokana na mfumo wa elimu uliopo nchini ambao haumsaidii kijana aliyemaliza shule ya sekondari au chuo kujiajiri mwenyewe.
Alisema mfumo wa elimu inayotolewa hapa nchini humdumaza mwanafunzi na kumfanya afikirie kuwa atakapomaliza elimu yake ni lazima aajiriwe na serikali, kitu alichodai kuwa si kweli.
“Serikali nayo sasa haina budi ifike wakati ibadilishe mifumo yake ya elimu kuanzia chekechea, elimu ya msingi, sekondari, vyuo vya elimu ya juu na vyuo vikuu, ili elimu inayotolewa katika shule zetu iweze kuwafanya vijana wanaomaliza shule kujiajiri wenyewe,” alisema Paresso.
Paresso alisema endapo mfumo wa elimu utabadilishwa na kuwafanya vijana wanaomaliza elimu yao kujiajiri kwa kiasi kikubwa tatizo la ukosefu wa ajira hapa nchini litapungua.
Hata hivyo aliwataka vijana hapa nchini kutobagua kazi na badala yake wafanye kazi yoyote iliyo halali ya kuwaingizia kipato ili kupunguza wimbi la vijana wasio na ajira nchini.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk. Ahmad Kanyama alisema tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana ni bomu ambalo linasubiriwa kulipuka na kwamba hatua za makusudi na za haraka zinatakiwa kuchukuliwa ili kujinusuru na hatari hiyo.
Aliongeza kusema kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana kwa sasa ni janga la kitaifa hivyo ni wajibu wa serikali kulitatua tatizo hilo kabla hakujatokea machafuko nchini.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment