na Danson Kaijage, Dodoma
SERIKALI imetangaza vita kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na uchakachuaji wa mbolea, mbegu na dawa ya kilimo na hivyo kuwasababishia wakulima hasara.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Adam Malima, alipokuwa akifafanua namna ya kukabiliana na wafanyabishara wasio waaminifu katika uuzaji wa mbolea.
Malima alisema ili kuhakikisha mapambano kati ya wafanyabiashara hao yanafanyika kwa ufanisi mkubwa, serikali imeunda chombo cha kudhibiti ubora wa mbolea.
Alisema chombo hicho ambacho kinafuatilia uthibiti wa mbolea kimeanza kufanya kazi na mbolea hiyo inafuatiliwa kuanzia kwa mkulima.
Malima aliongeza kuwa sababu ya kuunda chombo hicho ni matokeo ya wakulima kulalamikia upatikanaji wa mbolea ambayo haikidhi viwango na hivyo kuwalazimu kutumia fedha nyingi kununua mbolea pasipo kupata mavuno mazuri kama wanavyokusudia.
Aliongeza kuwa kitendo cha baadhi ya wafanyabiashara kusambaza mbolea feki kwa wakulima kimewasababishia hasara kubwa.
“Watanzania zaidi ya asilimia 75 wanategemea kilimo, wanategemea kupata mazao mengi kwa ajili ya chakula au biashara na kama mkulima anapata mbolea feki, hawezi kupata mazao mengi,” alisema.
Malima alifafanua kuwa dhana ya kilimo kwanza bila kuwa na udhibiti wa mbolea ni wazi kuwa itakuwa ndoto kwa wakulima kujikomboa katika umaskini.
Pamoja na kuwepo kwa sera ya ruzuku ya mbolea, pamekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwepo kuuziwa mbolea feki na kutoipata kwa wakati.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment