na Sitta Tumma, Mwanza
NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, amefichua madudu mengi yanayofanywa na kampuni ya huduma za meli, pamoja na Shirika la Reli Nchini (TRL), akisema kuwa mashirika hayo yamekubuhu kwa wizi wa mafuta ya kuendeshea meli na reli.
Alisema wizi huo mkubwa umekuwa ukifanywa na baadhi ya watumishi kwa kushirikiana na baadhi ya vigogo wa mashirika hayo wasiokuwa waaminifu, na kwamba hujuma hizo ni chanzo kikuu cha mashirika hayo kufa na kushindwa kujiendesha kwa ushindani wa kibiashara baina yake na sekta binafsi.
Kufuatia tuhuma hizo za wizi wa mafuta, Dk. Tizeba ameuagiza uongozi wa shirika la huduma za meli kupitia kwa Kaimu Meneja wake, Projest Samson Kanja kumfukuza kazi mara moja Kapteni mmoja ambaye aliwahi kukamatwa na lita 2,000 za mafuta ya wizi katika meli ya Mv. Victoria, inayofanya safari zake mikoa ya Mwanza na Kagera.
Akizungumza katika kikao cha pamoja na viongozi wa huduma za meli juzi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja kutembelea na kukagua shughuli za mashirika hayo, Dk. Tizeba alisema, kamwe serikali haiwezi kuvumilia hujuma za namna hiyo, kwani zimelenga kuichonganisha na wananchi wake.
Anazo taarifa sahihi kuhusu wizi huo wa mafuta ya meli na treni, ambao umekuwa ukifanywa kwa siri na wahusika punde wanapokuwa safarini na vyombo vyao, hivyo kusisitiza kapteni huyo afukuzwe kazi mara moja.
Kuhusu reli, Dk. Tizeba ambaye alikutana na wafanyakazi wa shirika hilo katika ofisi za makao makuu jijini hapa, licha ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwao, aliwarushia kombora zito la kuwataka waache wizi wa mafuta ya treni.
“Kule Marine kuna wizi mkubwa wa mafuta ya meli, Na hapa reli wizi wa namna hiyo upo tena mkubwa sana, Mnaiba mafuta mnapofika Imalampaka au Shinyanga,” alidai.
Aidha, Waziri Tizeba aliuagiza uongozi wa shirika hilo kuhakikisha unaanza kupeleka treni ya abiria jijini Mwanza hadi Dar es Salaam kabla ya Septemba mwaka huu, na kwamba mikakati hiyo ifanywe na uongozi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa shirika hilo, na si kutegemewa serikali.
Alisema mwaka huu wizara yake ilishatenga sh bilioni 18.9 kwa ajili ya kuifufua TRL, hivyo vichwa 18 vya treni vitakodishwa kutoka nchi ya Afrika Kusini, vichwa 13 vitanunuliwa vipya na 15 vitafufuliwa kwa ajili ya kufanya kazi zake.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment