na Happiness Mtweve, Dodoma
KITENDO cha Chama cha Mapinduzi (CCM), kumiliki viwanja mbalimbali vya michezo na kushindwa kuviendeleza kwa kuvikarabati na kuviweka kwenye mazingira mazuri jana kilivuta hisia za wabunge wengi na kufanya swali la msingi kupata maswali mengi ya nyongeza katika kipindi cha maswali na majibu.
Kutokana na hali hiyo ya CCM kushindwa kuviendeleza viwanja hivyo, serikali imetakiwa kuviondoa viwanja vyote ambavyo viko mikononi na vinamilikiwa na chama hicho kutokana na kushindwa kuviendeleza.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR -Mageauzi), wakati akiuliza swali la nyongeza.
Machali alisema viwanja hivyo ambavyo vinamilikiwa na CCM, vilijengwa na watu mbalimbali wakati wa chama kimoja, hivyo ni vema serikali ivirejeshe kwa watu hao ambao hivi sasa si Wana CCM.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala, alisema kuwa ni kweli viwanja hivyo vilijengwa wakati wa chama kimoja, hivyo kwa watu ambao si Wana CCM na walihusika kujenga viwanja hivyo, ni vema warudi CCM ili waweze kumiliki viwanja hivyo.
Swali la msingi liliulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya (CHADEMA ), ambaye alitaka serikali kuona umuhimu wa kurudisha viwanja 12 kwenye halmashauri husika, ili viwe sehemu ya mapato kwa halmashauri hizo, ambako kila mwanachi atafaidi matunda yake bila kujali itikadi yake.
Akijibu swali hilo, naibu waziri huyo alisema, serikali haina sababu za msingi za kuomba kuhamisha miliki ya viwanja 12 kutoka kwa wamiliki wake wa sasa na kuvikabidhi kwa halmashauri kama ilivyoshauriwa.
Makala alifafanua kuwa, viwanja 12 vinavyozungumzwa kwa sasa ni mali ya Chama cha Mapinduzi, ambapo kina vimiliki viwanja hivyo baada ya kufuata taratibu zote husika.
Alisema, serikali itakuwa tayari kuvipokea wakati wote kwa hatua zaidi kwa kutegemea sababu ya kuvikabidhi.
“Kwa kumbukumbu za wizara yangu, viwanja hivi hutumiwa na Watanzania wote bila kujali tofauti za kiitikadi na pia mamlaka za viwanja hivyo hulipa kodi mbalimbali kwa mamlaka za kodi za maendeleo husika, hivyo kuchangia pato katika mfuko wa serikali, fedha ambayo ni kwa ajili ya huduma mbalimbali ya jamii,” alisema Makala.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment