Home » » WATU MILIONI 11 TU KUPIGA KURA JUMAPILI

WATU MILIONI 11 TU KUPIGA KURA JUMAPILI

JUMLA ya Watanzania milioni 11.4 wamejiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Jumapili wiki hii, sawa na asilimia 62 ya lengo lililowekwa.
Katika uchaguzi huo, watakaochaguliwa ni wenyeviti wa vijiji na wajumbe wa halmashauri za vijiji, wenyeviti wa mitaa na wajumbe wa kamati za mitaa na wenyeviti wa vitongoji.
Mkoa wa Katavi umeongoza kwa kuandikisha asilimia 78 ya wapigakura huku mkoa wa Dar es Salaam umetajwa kufanya vibaya katika kuandikisha wapiga kura, ambapo waliojiandikisha ni asilimia 43 Pia katika uchaguzi huo wa Desemba 14, kutakuwa na ingizo jipya ambalo ni nembo ya chama ili kuwawezesha watu wasiojua kusoma na kuandika, kutambua kwa urahisi mtu wanayempigia kura.
Kwa walemavu ambao wako katika makundi maalumu, watalazimika kufika na ndugu zao, kwani ni marufuku kwa wasimamizi au walinzi au mtu yeyote anayehusika na uchaguzi, kumsaidia mpigakura kupiga kura yake.
Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Calist Luanda alisema hayo katika mkutano wake wa waandishi wa habari mjini hapa jana. Alisema katika uchaguzi huo, walitarajia kuandikisha wapigakura 18,587,742.
Alisema matarajio hayo yalipatikana, kutokana na taarifa za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, ambayo inaonesha asilimia 40 ya Watanzania wote wana miaka 18 na kuendelea.
Kati ya matarajio ya kuandikisha wapigakura 18,587,742, walioandikishwa ni 11,491,661, sawa na asilimia 62 ya matarajio,” alisema.
Alisema jukumu la serikali lilikuwa ni kuhamasisha wananchi wakajiandikishe na zaidi ya nusu ya watu waliotarajiwa kuandikishwa, wameandikishwa.
“Mkoa ulioandikisha Watanzania wengi ni Katavi asilimia 79 ya matarajio ukifuatiwa na mkoa wa Kagera asilimia 78,” alisema.
Alisema mkoa ambao haukufikia malengo chini ya asilimia 50 ni Dar es Salaam ulioandikisha asilimia 43 ya malengo yake, ukifuatiwa na Mkoa wa Kilimanjaro ulioandikisha asilimia 50.
Kwa upande wa halmashauri iliyovuka lengo ni Mpanda, iliyoandikisha asilimia 107 ya matarajio na halmashauri ya Babati asilimia 101 ya malengo waliyojiwekea.
Halmashauri zilizofanya vibaya ni Kilindi mkoani Tanga iliyofikia asilimia 21 ya matarajio na Same, mkoa wa Kilimanjaro asilimia 22 ya matarajio.
Alisema kutakuwa na karatasi za kura, ambayo itaandaliwa na halmashauri husika ambayo itakuwa na jina la mgombea, jina la chama, nembo ya chama na nembo ya halmashauri.
Alisema mpigakura atatakiwa kuweka alama ya tiki katika kisanduku kilichopo chini ya nembo ya chama, kuonesha kuwa amempigia kura mgombea aliyemtaka kumchagua.
Pia, vituo vya kupigia kura vinatakiwa kuwa wazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni ya siku ya kupiga kura, hivyo wapigakura watakaokuwepo kituoni saa 10 jioni, wataruhusiwa kupiga kura hadi watakapokuwa wamemaliza kupiga kura.
“Kutakuwa na sanduku maalumu la kupigia kura lililotengenezwa kwa namna itakayomwezesha mpiga kura na kutumbukiza kura yake kwa urahisi bila kuruhusu kura hiyo kutolewa ndani ya sanduku hilo,’’ alisema.
Alisema kabla ya kuanza kupiga kura, msimamizi wa uchaguzi atawaonesha wapigakura sanduku la kupigia kura lililo wazi na atalifungua kwa lakiri, kwa namna ambayo itazuia kufunguliwa bila kukata lakiri.
Alisema vitambulisho vitakavyotumika ni vitambulisho vya wapigakura uchaguzi mkuu, kitambulisho cha kazi kama mfanyakazi, hati ya kusafiria, kadi ya benki, kadi ya bima ya afya, kitambulisho cha shule kwa mwanafunzi mwenye miaka 18 na kuendelea, kitambulisho cha udereva au kitambulisho cha uraia.
Chanzo:habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa