Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango.
Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, amesema hatakubali kuruhusu misamaha ya kodi isiyokuwa na maslahi kwa taifa.
Alisema hayo jana bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la
Mbunge Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza, ambaye alisema ripoti
hazionyeshi faida ambayo serikali inazipata kutokana na misamaha ya
kodi, hasa kwenye kampuni za uwekezaji katika sekta ya madini.
“ je serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kampuni hizi
zinaondolewa kwenye misamaha ya kodi na kuanza kulipa kodi ili wajibu wa
kutoa huduma za jamii ubakie kwa serikali?,” alihoji Peneza.
Akijibu, Dk. Mpango alisema wizara yake imeongeza vitengo vya
kukagua misamaha ya kodi ili kuhakikisha misamaha ya kodi
itakayoruhusiwa ni ile tu yenye faida kwa taifa.
Alisema misamaha ya kodi ambayo imekuwa ikitolewa kwenye kampuni za
madini imepungua kutoka takribani asilimia 17.6 ya kodi zote zinatolewa
na kufikia asilimia tisa.
Alisema hatua zilizochukuliwa ni kurekebisha sheria za kodi na
wabunge walipitisha marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongeleko la Thamani
ambayo iliondoa misamaha mingi ya kodi.
Alisema misamaha ya kodi ni asilimia 56 ya mapato ya kodi zote na
kwamba maboresho ya sheria hiyo ya misamaha ya kodi imesaidia kupungua
kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.
Aidha, Dk. Mpango alisema wanafanya jitihada kubwa kushughulikia
mazingira ya biashara na uwekezaji, kwa kuwa uwekezaji hautegemee kodi
peke yake.
Awali, akijibu swali la msingi la Mbunge huyo, Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema misamaha ya kodi ni
moja ya vivutio vinavyotolewa kuwahamasisha wawekezaji waichague
Tanzania.
Hata hivyo, alisema serikali inatambua mapungufu yaliyoko katika kutumia kodi kama kivutio cha uwekezaji.
“Tatizo kubwa ni wale wanaotumia fursa hii kuhujuma mapato ya
serikali pale misamaha inaposababisha kutokuwapo na ushindani sawa kati
ya kampuni moja na nyingine, lakini serikali itaendelea kufanya
maboresho ya sheria ili kupunguza misamaha ya kodi,” aliongeza kusema.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment