Home » » Waziri Mkuu kuongoza maziko ya Askofu Isuja

Waziri Mkuu kuongoza maziko ya Askofu Isuja

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo anatarajiwa kuongoza maziko ya aliyekuwa Askofu wa kwanza mzalendo wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Mathias Joseph Isuja yatakayofanyika kwenye Kanisa Kuu la Paulo wa Msalaba.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maziko hayo, Peter Mavunde, Waziri Mkuu anatarajiwa kuwasili Kanisa Kuu la Jimbo la Mtakatifu Paulo wa Msalaba kuanzia saa 4:30 asubuhi.
Ibada ya maziko inatarajiwa kuanza saa 4:30 za asubuhi na itaongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya akisaidiana na Rais wa Baraza la Maskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Tarcius Ngalalekumtwa pamoja na maaskofu wengine.
Taarifa hiyo ilieleza zaidi kwamba pia Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ni miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kuhudhuria maziko hayo.
Askofu Isuja aliyezaliwa Agosti 14, 1929 katika kijiji cha Haubi wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma, alifariki dunia Aprili 12, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 86.
Alifia katika Hospitali ya Mtakatifu Gaspari Itigi Manyoni mkoani Singida alikokuwa akitibiwa saratani ya tumbo.
Alipata daraja la upadri akiwa na umri wa miaka 31 na baadaye mwaka 1972 aliteuliwa kuwa Askofu wa kwanza mzalendo wa Jimbo Katoliki la Dodoma akiwa na miaka 41 na kuendelea na utumishi wake katika kanisa hadi alipostaafu Januari 15, 2005 akiwa na umri wa miaka 75.
Waumini wa kanisa Katoliki jimboni humo jana waliupokea mwili wa marehemu Askofu Isuja kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako mamia ya waombolezaji walijipanga kuanzia eneo la Tambuka Reli katika makutano ya barabara ya Nyerere na ile iendayo Posta wakiusindikiza mwili huo hadi ndani ya Kanisa Kuu.

 Chanzo Gazeti la Habari leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa