Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Askofu Mkuu wa Jimbo la Dodoma ,
Beatus Kinyaiya katika mazishi ya Askofu Mstaafu wa Dodoma Mathias Isuja
yaliyofanyika kwenye kanisa kuu la Mtakatifu Paul wa Msalaba Mjini
Dodoma Aprili 20, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa Askofu Mstaafu wa
Jimbo Kuu la Dodoma, Mathias Isuja katika mazishi yaliyofanyika kwenye
Kanisa Kuu la Mtakatifu Paul wa Msalaba Aprili 20, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye kaburi la Askofu
Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mathias Isuja katika mazishi
yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Paul wa Msalaba, Aprili
20, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya waumini na wakazi wa mkoa wa
Dodoma katika mazishi ya Mhashamu Askofu Mstaafu, Mathias Isuja wa
Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma.
Amesema kifo hicho ni pigo kwa watu wote na si kwa kanisa pekee kwa sababu walimtegemea kulisaidia Taifa kiroho na kimaendeleo.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 20, 2016) wakati akizungumza
na waumini na wakazi wa mkoa huo na mikoa jirani kwenye ibada ya mazishi
iliyofanyika kwenye Kanisa la Kiaskofu la Mtume Paulo wa Msalaba mjini
Dodoma.
Askofu
Isuja ambaye alizaliwa Agosti 14, 1929 alikuwa Askofu wa kwanza
mzalendo katika Jimbo la Kanisa Katoliki la Dodoma. Alistaafu kazi ya
uaskofu mwaka 2004 kwa mujibu wa sheria ya kanisa. Alifariki Aprili 13,
mwaka huu.
Waziri
Mkuu amesema Serikali itaendelea kumuenzi Askofu Isuja kwa kazi nzuri
aliyoifanya wakati wa uhai wake na kuyaendeleza yote aliyoyaanzisha
kwenye maeneo aliyowahi kuyatumikia.
“Tumepoteza
mtu makini, sisi ni mashahidi wa mchango mkubwa wa marehemu siyo tu
katika kutoa huduma za kiroho, bali pia huduma za kijamii zilizolenga
kuleta maendeleo kwa wananchi katika jimbo hili la Dodoma na katika
taifa kwa ujumla,” amesema.
Mapema,
akitoa mahubiri wakati wa ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la
Mwanza, Mhashamu Judathadeus Ruwa’ichi alisema waumini wa kanisa hilo wa
mkoa wa Dodoma na Tanzania nzima wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu
kwa maisha marefu aliyomjalia Askofu Isuja.
“Tunapaswa
kumshukuru kwa maisha marefu ambayo Mungu alimzawadia baba yetu Isuja.
Katika Zaburi ya 90 tunasoma kuwa mwanadamu ana miaka ya matazamio
ambayo ni 70, lakini yeye alipewa miaka ya matazamio 70 na akazawadiwa
nyongeza ya miaka 10 na kisha miaka mingine sita na nusu,” alisema.
Alisema
zawadi nyigine ambayo Mungu aliwapatia waumini hao ni ya imani ambayo
Baba Askofu Isuja aliipokea, aliifundisha na aliishi na akawataka
waendelee kumshukuru Mungu kwa hilo. “Miaka 56 ya utumishi wake kama
padre na askofu ni zawadi kwa Dodoma na Tanzania na siyo kwake yeye
binafsi,” alisema.
Ibada
hiyo ya mazishi ilihudhuriwa na Maaskofu Wakuu na Maaskofu wa kawaida 28
kutoka majimbo ya Dodoma, Mwanza, Mbeya, Njombe, Mpanda, Iringa,
Songea, Tabora, Morogoro na Mahenge. Mengine ni Musoma, Rulenge, Mbinga,
Moshi, Same, Kahama, Sumbawanga, Shinyanga, Mtwara na Lindi. Majimbo
mengine ni Bukoba, Tanga, Singida, Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha,
Kondoa na Kayanga.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980.
DODOMA.
JUMATANO, APRILI 20, 2016.
0 comments:
Post a Comment