Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo anatarajiwa kuongoza maziko ya
aliyekuwa Askofu wa kwanza mzalendo wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la
Dodoma, Mhashamu Mathias Joseph Isuja yatakayofanyika kwenye Kanisa Kuu
la Paulo wa Msalaba.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maziko hayo, Peter Mavunde,
Waziri Mkuu anatarajiwa kuwasili Kanisa Kuu la Jimbo la Mtakatifu Paulo
wa Msalaba kuanzia saa 4:30 asubuhi.
Ibada ya maziko inatarajiwa kuanza saa 4:30 za asubuhi na itaongozwa
na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya
akisaidiana na Rais wa Baraza la Maskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Tarcius
Ngalalekumtwa pamoja na maaskofu wengine.
Taarifa hiyo ilieleza zaidi kwamba pia Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu,
Benjamin Mkapa ni miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kuhudhuria maziko
hayo.
Askofu Isuja aliyezaliwa Agosti 14, 1929 katika kijiji cha Haubi
wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma, alifariki dunia Aprili 12, mwaka huu
akiwa na umri wa miaka 86.
Alifia katika Hospitali ya Mtakatifu Gaspari Itigi Manyoni mkoani Singida alikokuwa akitibiwa saratani ya tumbo.
Alipata daraja la upadri akiwa na umri wa miaka 31 na baadaye mwaka
1972 aliteuliwa kuwa Askofu wa kwanza mzalendo wa Jimbo Katoliki la
Dodoma akiwa na miaka 41 na kuendelea na utumishi wake katika kanisa
hadi alipostaafu Januari 15, 2005 akiwa na umri wa miaka 75.
Waumini wa kanisa Katoliki jimboni humo jana waliupokea mwili wa
marehemu Askofu Isuja kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako
mamia ya waombolezaji walijipanga kuanzia eneo la Tambuka Reli katika
makutano ya barabara ya Nyerere na ile iendayo Posta wakiusindikiza
mwili huo hadi ndani ya Kanisa Kuu.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment