Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Mpango akitoa hotuba katika mkutano wa uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo
wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma
kilichofanyika mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango
akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo wa
Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma, kushoto
ni Katibu tawala wa mkoa wa Dodoma bibi. Rehema Madenge na kulia ni bi Anna
Kimwela kutoka Tume ya Mipango.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Mpango akionesha kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na
Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma (Public Investment
Management Operational Manual), kulia ni Kaimu katibu mtendaji wa Tume ya
Mipango Bibi Florence Mwanri na kushoto ni katibu tawala wa Mkoa wa Dodoma Bibi
Rehema Madenge.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Mpango (wa tano kutoka kushoto kwa waliokaa) akiwa katika picha ya
pamoja na wajumbe wa mkutano mara baada ya uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo
wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma.
Na Adili Mhina, Dodoma
Tume ya
mipango imezindua kitabu cha Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya
Uwekezaji katika sekta ya Umma (Public Investment Management Operational
Manual) kwa lengo la kuimarisha utendaji, uwajibikaji na kuleta ufanisi katika
matumizi ya rasilimali za umma zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Akizindua
mwongozo huo katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa juma mjini Dodoma na
kuhudhuriwa na wataalamu wa uchumi, sera na mipango kutoka wizara, halmashauri
na taasisi mbalimbali za serikali,
Waziri wa fedha na mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango alieleza kuwa shabaha
ya mwongozo huo ni kutoa maelekezo ya mchakato na hatua zinazohitajika kufuatwa
katika kutayarisha na kutekeleza miradi yote inayotumia fedha za umma au kwa
kushirikiana na sekta binafsi.
Waziri
mpango aliwataka viongozi wote wenye dhamana ya kusimamia miradi kusoma
mwongozo huo na kuuelewa ili kuepuka makosa yaliyokuwa yakijitokeza huko nyuma
huku akisisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano haitamvumilia wala kumonea
huruma mtendaji yeyote atakayeshindwa kuwajibika ipasavyo.
“Kuanzia
sasa watu ambao wamepewa dhamana ya kusimamia miradi ya maendeleo, miradi
itakaposhindwa kuna mambo mawili tu yakufanya; ama waachie ngazi mapema wao
wenyewe au basi wasubiri tuwatumbue. Kwahiyo nawaombeni sana hiki kitabu
ambacho kimeandaliwa kuanzia leo kila mmoja akisome vizuri ili kusiwe na miradi
tena ambayo ni ya ovyo ovyo,” alisisitiza waziri mpango.
Mwongozo huo unazielekeza Wizara, Idarana Wakala wa Serikali,Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa jinsi ya kufanya uchambuzi unaozingatia vigezo vya
kiuchumi na kifedha na kufafanua mbinu, hatua, taratibu, na kuweka
viwango vinavyohitajika katika kuandaa na kuwekeza miradi.
Waziri Mpango alieleza kuwa maelekezo ya mwongozo huo yanafafanua vigezo muhimu vya uchambuzi wa kiuchumi na kifedha ili kufikia uamuzi
wa miradi ipi ina manufaa na inaweza kupata mikopo katika soko la mitaji la
ndani au la kimataifa.
“Mwongozo
huu umeanisha vigezo kama mzunguko wa mradi (project cycle) ikiwa ni pamoja na
andiko la awali (concept note), mchanganuo wa faida na hasara (cost-benefit
analysis) vigezo vya kuchanganua mradi kama vile uwezo wa uzalishaji (internal
rate of return) na thamani halisi ya uwekezaji (Net Present
Value), na vinginevyo”Alieleza Dr. Mpango.
Kuzinduliwa kwa mwongozo huo kunatoa tafsiri kuwa miradi yote itakayohitaji
fedha za Serikali katika Bajeti italazimu kufuata utaratibu uliobainishwa katika kitabu hicho
ili kuweza kuimarisha ufanisi na kupata thamani ya fedha. Hivyo,
Mwongozo ni chombo muhimu katika michakato mbalimbali ya
kupanga bajeti kama vile Mwongozo wa Mpango na Bajeti, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka Mmoja na kadhalika.
Kwa upande wake Kaimu katibu mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi Florence
Mwandri alieleza kuwa mwongozo huo unategemewa
kuwa mwanzo wa kujenga uwezo katika usimamizi wa uwekezaji wa umma na utakuwa
ni msingi wa kuwaimarisha maafisa wa serikali kinyenzo katika kuchambua,
kuchagua, kuwasilisha miradi ya uwekezaji kiuchumi na kifedha, pia kijamii kwa kukidhi
taratibu na sheria zinazoendesha uwekezaji katika sekta ya umma.
“Katika kufanikisha utekelezaji wa Mwongozo huu na kujenga uwezo wa
kutosha, Serikali imedhamiria kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo kwa walengwa
wakuu katika ngazi za mafunzo ya muda mfupi, muda wa kati na mrefu ili kuongeza
utaalam na kuwekeza miradi michache kwa mwaka wa bajeti lakini kwa ufanisi
zaidi”, alisema bibi Mwanri.
Mwongozo huo pia unatoa taratibu kwa miradi ambayo haitapata fedha kwa
mwaka husika itawekwa katika kanzi-data (Database) ambayo itaanzishwa chini ya
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kwa ajili ya kufikia malengo ya utekelezaji wa
usimamizi wa uwekezaji katika sekta ya umma.
Kukamilika kwa kanzi-data kutasaidia wadau mbalimbali wanaohusika na
maamuzi ya uwekezaji katika sekta ya umma kuwa na uelewa mmoja kuhusu miradi
yenye kipaumbele. Kanzi-data itaonesha miradi gani ya umma, inategemewa
kutekelezwa, itaanza lini, na kumalizika lini na ina fedha kiasi gani.
0 comments:
Post a Comment