Mkuu wa shule ya sekondari Central Dodoma Bw. Kennedy Kagala (Kushoto) akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi (katikati) kitabu cha kumbukumbu za walimu wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa shuleni hapo. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Betty Mkwasa.
Mkuu wa shule ya sekondari Central Dodoma Bw. Kennedy Kagala (Kushoto) akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi (Katikati) kitabu cha kumbukumbu ya walimu wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa shuleni hapo. kulia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Betty Mkwasa.
Mwalimu Peter Mzanji (kushoto) aliyeajiriwa kwa muda - part time akielezea jambo kwa mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dr. Rehema Nchimbi (wa pili kushoto) wakati alipofanya ziara shule ya sekondari Central Dodoma . anayemfuatia Mkuu wa Mkoa ni Mkuu wa Shule Bw. Kennedy Kigala, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Betty Mkwasa na Mkaguzi Mkuu wa Shule Kanda ya Kati Bi.Regina Arevo. Picha zote na Jeremia Mwakyoma - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
===== ========= ======== ======
TAARIFA YA ZIARA YA KUSHTUKIZA YA MKUU WA MKOA WA DODOMA MHE. DR. REHEMA NCHIMBI (MNEC) KATIKA SHULE YA SEKONDARI CENTRAL DODOMA TAREHE 27 MACHI, 2012.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dr. Rehema Nchimbi jana amefanya ziara ya kushtukiza kwenye shule ya sekondari Central iliyopo Mjini Dodoma kufuatia malalamiko kadhaa juu ya shule hiyo aliyoyapata kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo wanafunzi.
Lengo la ziara hiyo ya Dr. Nchimbi ambayo aliongozana na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Betty Mkwasa, Mkaguzi Mkuu wa shule Kanda ya Kati Bi. Regina Arevo na Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Dodoma Bi. Suma Mwampula ilikuwa kupata picha halisi ya malalamiko yaliyotolewa na kutafuta namna ya kuyashughulikia.
Miongoni mwa matatizo aliyopokea Mkuu wa Mkoa juu ya shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha sita ni pamoja na kutokuwa na walimu walioajiriwa rasmi/masharti ya kudumu badala yake shule inatumia walimu wa muda (part time). Malalamiko mengine ni kuwa shule hiyo haina mhasibu wala akaunti ya benki. Aidha ilielezwa kuwa shule hiyo haina bodi na kama ipo basi haikai vikao na kusimamia shule ipasavyo, vilevile shule ina tatizo la ufaulu mdogo wa wanafunzi kwenye mitihani ya Taifa hali kadhalika tatizo la ubovu na uchakavu wa miundombinu mbalimbali.
Katika ziara hiyo Mhe. Mkuu wa Mkoa na Ujumbe alioambatana nao waliweza kubaini kuwapo kwa matatizo hayo. Vilevile waliweza kubaini kuwa hakukuwa na taarifa, kumbukumbu muhimu za walimu wala mikataba ya ajira.
Akijibu baadhi ya hoja Mkuu wa shule hiyo ambaye pia ndio mmiliki wa shule Bw. Kennedy Kigala alisema kuwa shule yake inamhasibu ambaye kabla ya kuwa mhasibu alikuwa katibu Muhtasi wake hivyo alifundishwa kazi za uhasibu shuleni hapo na kuanza kufanya kazi hiyo. Vilevile walimu wako 28 wakiwamo wa masharti ya kudumu na wa muda na kuongeza mfumo wa kuajiri walimu wa muda unawawezesha kulipa walimu kulingana na vipindi walivyofundisha.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa shule kanda ya kati Bi. Regina Arevo alisema kuwa ukaguzi wa mwisho shuleni hapo ulifanyika mwezi Februari mwaka huu na pamoja na malalamiko yaliyofikishwa kwa Mkuu wa Mkoa, walibaini usimamizi wa taaluma uko chini sana na katika ngazi za ufaulu shule hiyo imepata daraja D. Idadi ya walimu ni 28 ambapo watano ni wakudumu na 23 ni wa muda.
Aliongeza kuwa shule hiyo ni miongoni mwa shule sumbufu katika mkoa wa Dodoma na baada ya ukaguzi huo wa Februari waliagiza mapungufu yote yashughulikiwe kabla ya ukaguzi ujao wa mwezi Aprili na endapo shule hiyo itashindwa kuyashughulikia matatizo hayo basi haitaruhusiwa kupokea tena wanafunzi wa kidato cha kwanza na mwisho shule hiyo itafungwa.
Baada ya kujiridhisha na hali halisi ya shule hiyo Mkuu wa Mkoa alitoa muda wa mwezi mmoja kwa shule hiyo kuhakikisha inashughulikia na kumaliza matatizo yalioonekana. Miongoni mwa mapungufu aliyomuagiza Mkuu wa shule hiyo ambaye ndio mmiliki kuyashughulikia ni pamoja na kuhakikisha shule inakuwa na mhasibu tena mwenye sifa na elimu ya uhasibu, kuhakikisha shule ina idadi ya kutosha ya walimu wa kudumu kulingana na masharti ya usajili wa shule, kuwe nataarifa na kumbukumbu sahihi na uhakika pamoja na mikataba ya walimu wa aina zote (wa kudumu na wa muda).
Vilevile Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa shule kuitisha kikao cha bodi mara moja ili kupanga mikakati ya kutatua matatizo hayo na kuagiza bodi hiyo pamoja na kazi nyingine kuandaa kikao cha wazazi ili wajue mazingira na matatizo ya shule wanayosoma watoto wao na katika vikao vyote vya bodi Mkaguzi wa Shule na Afisa Elimu washirikishwe, vilevile amewaagiza watendaji hao kuisimamia kwa karibu shule hiyo iweze kuyashughulikia matatizo hayo ndani ya mwezi mmoja na ameahidi atafanya ziara nyingine shuleni hapo baada ya mwezi mmoja.
Dr. Nchimbi aliongeza kuwa Serikali hivi sasa inaunga mkono ushirikikiano baina ya taasisi za umma na binafsi katika kutoa huduma na kusema shule hiyo haina budi kufanya mabadiliko ili iweze kubeba dhamana ya kuwa Dodoma ambayo ni Makao Makuu ya Nchi.
Imetolewa na:
Idara ya Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
DODOMA
28 Machi, 2012
0 comments:
Post a Comment