Mnamo
tarehe 22/04/2012 majira ya saa 13:15 mchana katika eneo la Kibaigwa
Wilaya ya Kongwa, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata Mirungi bunda
ishirini na nne (24), yenye thamani ya shillingi laki moja na kumi na
saba elfu.
Katika tukio hilo watu wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani
humo kwa tuhuma za kukutwa na mirungi hiyo, watuhumiwa hao ni ABDUL S/O
AHMED FARAH, Maarufu kama CHIFU, mwenye umri wa miaka (40), na OMARY
S/O HASH FARAH miaka (50) wote wakazi wa Kibaigwa.
Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa toka kwa wananchi kuwa kuna
watu wanafanya biashara ya kuuza Mirungi, ndipo Polisi waliweka mtego
na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja Bw. OMARY S/O HASH FARAH akiwa
na ruba moja (bunda moja) alilokuwa anataka kuliuza kwa mtu aliyewekwa
kama mtego.
Aidha Baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, ndipo mtuhumiwa mwenzake
akajifungia chumbani ili asikamatwe, lakini baada ya kukamatwa na
alipopekuliwa akakutwa na ruba nyingine ishirini na tatu (23) ndani ya
nyumba walimokuwa wakiishi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linapenda kutoa pongezi kwa wananchi,
waliohusika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu hao, ambao kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi walifanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa
hao.
Mwisho napenda kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutekeleza dhana
nzima ya Polisi Jamii na Ulinzi shirikishi, ili kuhakikisha maeneo yetu
tunayoishi yanakuwa ya Utulivu, Amani na Salama na hivyo kusaidia
kukuza ustawi wa jamii yetu.
Wakati huo huo, mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la JOHN S/O LUGANJE,
mwenye umri wa miaka hamsini na nne(54) mgogo, na mkulima mkazi wa
kijiji cha chunju wilaya ya Mpwapwa amekutwa amekufa porini baada ya
kujinyonga kwa shati alilokuwa amelivaa.
Kwa mujibu wa Taarifa za Jeshi la Polisi Wilayani Mpwapwa, marehemu
aligundulika amekufa porini majira ya saa nane mchana, siku ya jumamosi
tarehe 21/04/2012, na kwamba alikuwa ametoweka nyumbani kwake toka
tarehe 16/04/2012.
Hata hivyo taarifa toka kitongoji cha Ng’ongwa katika kijiji cha Chunyu
zinasema marehemu alikuwa mgonjwa wa akili, hata hivyo Jeshi la polisi
linaendelea na upelelezi wa tukio hilo.
Imetolewa na: SACP - Zelothe Steven
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma

0 comments:
Post a Comment