Home » » HOJA YA KUTOKUWA NA IMANI NA WAZIRI MKUU BUNGENI KWA MUJIBU WA KATIBA IBARA YA 53A NA KANUNI YA BUNGE, KIFUNGU CHA 133 KUWASILISHWA KWA SPIKA KESHO TAREHE 23/04/2012

HOJA YA KUTOKUWA NA IMANI NA WAZIRI MKUU BUNGENI KWA MUJIBU WA KATIBA IBARA YA 53A NA KANUNI YA BUNGE, KIFUNGU CHA 133 KUWASILISHWA KWA SPIKA KESHO TAREHE 23/04/2012






 Mbunge wa Kigoma Kaskazin(Chadema)na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC),Zitto Kabwe




 ----


HOJA YA KUTOKUWA NA IMANI NA WAZIRI MKUU BUNGENI KWA MUJIBU WA KATIBA IBARA YA 53A NA KANUNI YA BUNGE, KIFUNGU CHA 133 KUWASILISHWA KWA SPIKA KESHO TAREHE 23/04/2012

•    Masharti yametimizwa; wabunge 73 wazalendo wamesaini
•    Ni mwendelezo wa ‘Operesheni Uwajibikaji’

Mnamo
tarehe 19/04/2012 wakati nahitimisha hoja ya Kamati ya Bunge ya
Mashirika ya Umma nilieleza kusudio langu la kuwaomba waheshimiwa
wabunge waniunge mkono katika kutia saini zisizopungua asilimia 20
yawabunge wote ili kuweza kutimiza matakwa ya Katiba ibara ya 53A kwa
ajili ya kuwasilisha Bungeni hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.

Mnamo
tarehe 20/04/2012 niliandaa orodha ya waheshimiwa wabunge wote na
kuisambaza ndani na nje ya ukumbi wa Bunge ili waheshimiwa wabunge wote
waweze kutia saini hizo, na mpaka leo tarehe 22/04/2012 orodha hiyo
imetimiza idadi ya wabunge wazalendo wanaopigania uwajibikaji 73 kutoka
vyama vyote vyenye uwakilishi Bungeni, isipokuwa chama cha UDP ambacho
kina Mbunge 1 na hajatia saini waraka huo mpaka sasa. 



Kwa mujibu
wa kanuni za Bunge kifungu
cha 133 (1) kinasomeka “Mbunge yeyote anaweza kutoa taarifa ya
maandishi kwa Spika ya kutaka kuleta hoja ya kutokuwa na imani na Waziri
Mkuu kwa mujibu wa ibara ya 53A ya Katiba” na kwa mujibu wa kifungu
kidogo cha (3) kinasomeka “hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri
Mkuu haitajadiliwa na Bunge
isipokuwa tu kama;

(a) 
“taarifa ya maandishi iliyowekwa saini na kuungwa mkono na Wabunge
wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote itatolewa kwa Spika, siku
zisizopungua kumi na nne kabla ya siku inayokusudiwa kuwasilishwa
Bungeni;”

Hali
kadhalika kanuni za Bunge Kifungu cha 133 (4) kinasomeka kuwa “hoja
inayotolewa chini ya Kanuni hii na iliyotimiza masharti ya
Katiba,itawasilishwa Bungeni mapema iwezekanavyo na itaamuliwa kwa kura
za siri”.

Hivyo
basi baada ya kutimiza matakwa ya kikatiba na kanuni za Bunge kesho
tarehe 23/04/2012 tutawasilisha rasmi kwa Spika Taarifa ya Maandishi kwa
mujibu wa kanuni 133 (1) na (3) ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri
Mkuu kwa kushindwa kusimamia uwajibikaji wa Serikali Bungeni kwa mujibu
wa ibara ya 52 na hivyo kulinda Mawaziri wenye kusababisha matumizi
mabaya ya fedha za umma na kulisababishia hasara taifa.

Tunatarajia
kwamba siku kumi na nne baada ya kuwasilisha hoja hiyo Bunge litakutana
kwa  haraka kujadili hoja hiyo ili kuwezesha uwajibikaji na hatua
kuchukuliwa za kuhakikisha mapendekezo ya ripoti za Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) na maazimio ya Bunge
yanatekelezwa. Hoja hii
ni mwendelezo wa ‘Operesheni Uwajibikaji’ hivyo tunaomba wabunge
wazalendo na watanzania wote waiunge mkono ili kuimarisha Uwajibikaji wa
Viongozi, kupambana na ubadhirifu na kunusuru uchumi wa nchi na
kuchangia katika ustawi wa wananchi.

Kwa niaba ya wabunge wazalendo waliotia saini kuunga mkono taarifa ya
hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ni;

  …………………………….
Kabwe Zuber Zitto.
Mbunge Jimbo la Kigoma Kaskazini.
22/04/2012.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa