Happiness Mtweve, Dodoma
MTENDAJI wa Kampuni ya MMI Steel Resources, Subhash Patel, amepongezwa kwa juhudi zake za kuhakikisha kuwa mradi wa makaa ya mawe na chuma wa Liganga na Mchuchuma unaanza kufanya kazi mapema iwezekanavyo katika muda wa makubaliano.
Pongezi hizo zimetolewa na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), mjini hapa jana alipokuwa akitoa taarifa kwa wabunge wenzake, waliotaka kujua hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo utakaozalisha tani 330,000 za chuma ghafi katika hatua ya kwanza.
“Kazi aliyoifanya Subhash ya uchorongaji wa miamba kwa lengo la kubaini uwingi na ubora wa madini ya makaa ya mawe na chuma cha Maganga Matitu ni kubwa sana. Jumla ya mashimo 58 (mita 11,298) yamechimbwa Liganga na mengine 28 (mita 4,547) yamechimbwa Katewaka na sampuli zake kupelekwa maabara,” alisema Filikunjombe.
Alisema sampuli za chuma na makaa ya mawe zilizopelekwa Canada, Uingereza, Ireland na Afrika Kusini, zinaonesha ubora unaofaa na kwamba kazi ya usanifu wa migodi ya chuma na makaa ya mawe imeshaanza.
Filikunjombe, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, alisema juhudi za mwekezaji huyo zitasaidia kuanza kwa ujenzi wa kiwanda pamoja na mgodi mapema mwaka 2013 ili uzalishaji wake uwe umekwishaanza mwezi Oktoba 2014.
“Mradi huu utaongeza sana kasi ya maendeleo katika Wilaya ya Ludewa na Tanzania kwa ujumla, kwa vile mwekezaji ameandaa mkakati wa kuwawezesha wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi waweze kunufaika na shughuli za mradi kwa lengo la kuinua kipato cha wana Ludewa na kuondoka umaskini wao, kwani utatoa ajira kwa wafanyakazi 11,000,” alisema.
Filikunjombe ameitaka serikali itoe fedha kiasi cha sh 1.7 bilioni kwa ajili ya upanuzi wa barabara toka Njombe hadi Ludewa ili kuwawezesha wawekezaji kupitisha vifaa pamoja na mitambo mizito kwenda migodini, na kwamba lazima barabara ya Njombe hadi Manda, Ludewa pia ijengwe kwa kiwango cha lami.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment