Mwandishi Wetu, Dodoma
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeongeza fedha za kusaidia Ofisi za Wakaguzi wa Elimu ya Msingi na Sekondari pamoja na kupunguza matatizo katika Shule za Sekondari za Kata katika mwaka wa fedha 2012/13.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alibainisha hayo jana wakati akijibu maswali ya wabunge wa viti maalumu, Elizabeth Batenga (CCM) na Lucy Owenya(Chadema), ambao walitaka kujua mikakati ya wizara hiyo kukabiliana na matatizo ya uhaba wa wakaguzi katika shule ya sekondari na msingi.
Wabunge hao pia walitaka kujua mkakati wa Seikali kuhusu tatizo la walimu ambao pia wengi hukimbilia shule binafsi, pamoja na uhaba wa mahitaji muhimu katika shule hizo.
Akijibu swali hilo Mulugo alisema, wizara hiyo inatambua matatizo katika sekta ya elimu na hivyo, itajitahidi kuyapunguza kwa njia mbalimbali ikiwamo kuongeza fedha za katika ofisi za wakaguzi.
Alisema kuwa nyongeza ya fedha hizo itasaidia wakaguzi hao kukagua shule hizo akiongeza pia kwamba shule zenye mapungufu zilipewa vibali vya muda ili kuanza kutatuliwa matatizo yao.
“Utoaji na ukaguzi wa elimu katika shule na vyuo vya Serikali na visivyo vya Serikali, unasimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taasisi zake ikiwemo Idara ya Ukaguzi wa Shule, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Tume ya Vyuo Vikuu,”alisema Mulugo.
Akizungumzia tatizo la walimu, Mulugo alisema Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 1995, inafafanua wazi kuwa utoaji wa elimu nchini utakuwa wa ushirikiano wa shule za Serikali na sekta binafsi ambapo kuhusu suala la mikataba hasa kwa walimu waliomeshwa na Serikali alisema suala hilo linaweza kuzungumzika.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment