na Happiness Mtweve, Dodoma
SERIKALI imesema deni la taifa limeongezeka kutoka sh trilioni 17.6 kwa kipindi cha Machi 2011 hadi kufikia sh trilioni 20.3 katika kipindi kilichoishia Machi 2012, sawa na asilimia 15.4.
Hayo yalibainishwa bungeni mjini hapa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano, Stephen Wassira, wakati alipokuwa akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2011 na mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2012/13.
Akifafanua zaidi kuhusiana na deni hilo, Wassira alisema kati ya fedha hizo, sh bilioni 15 ni deni la nje na sh bilioni 12 ni deni la umma, wakati kiasi kilichosalia ni deni la sekta binafsi.
Alisema hadi kufikia Machi mwaka huu, deni la ndani lilifikia sh trilioni 4.97 ikilinganishwa na sh trilioni 4.497 kwa kipindi cha Machi 2011, sawa na ongezeko la asilimia 10.5.
“Mwaka 2011, serikali ilitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kikanda ikiwamo ujenzi wa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 90,” alisema waziri.
Kwa upande wa maendeleo katika sekta za kiuchumi na kijamii alisema shughuli za kiuchumi za kilimo zinazojumuisha mazao, mifugo, misitu na uwindaji zilikua kwa kiwango cha asilimia 3.6 kwa mwaka 2011 kutoka asilimia 4.2 kwa mwaka 2010.
“Upungufu huo ulitokana na kuchelewa kwa mvua za msimu kwa mwaka 2009/10 na kuathiri uzalishaji wa mazao, ambapo mchango wa shughuli za kiuchumi za kilimo ulikuwa asilimia 23.7 ya pato la mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 24.1 mwaka 2010,” alisema Wassira.
Katika eneo la viwanda na ujenzi, Wassira alisema shughuli za kiuchumi katika sekta hiyo zilikua kwa kiwango cha asilimia 6.9 kwa mwaka 2011 kutoka asilimia 8.2 kwa mwaka 2010 na kuongeza pato la Taifa kutoka asilimia 22.4 kwa mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 22.7 kwa mwaka 2011.
Alisema shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani zilikua kwa kiwango cha asilimia 7.8 kwa mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 7.9 kwa mwaka 2010 wakati katika sekta ndogo ya ujenzi ilikua kwa kiwango cha asilimia 9.0 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 10.2 kwa mwaka 2010.
Katika masuala mtambuka, Waziri Wasira, alisema kutokana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, inakadiriwa kuwa idadi ya watu na makazi hapa nchini kwa mwaka 2011 iilikuwa milioni 44.5 ikilinganishwa na milioni 43.2 kwa mwaka 2010.
Alifafanua kuwa katika idadi hiyo wanaume walikuwa milioni 21.9 na wanawake milioni 22.6, sawa na asilimia 50.7 huku Tanzania Bara ikikadiriwa kuwa na watu milioni 43.2 sawa na asilimia 97.0 na Tanzania Zanzibar watu milioni 1.3, ambapo mgawanyo wa watu unaonesha kuwa asilimia 73.3 wanaishi vijijini wakati asilimia 26,7 ya watu wanaishi mjini.
“Hususan katika viashiria vya afya vifo vya watoto wachanga na walio na umri wa chini ya miaka mitano vimeendelea kupungua japo kwa kasi ndogo ambayo haiwezi kufikia malengo ya milenia,” alisema Wassira.
Kuhusiana na hatua za kudhibiti malaria mwaka 2011, Serikali ilisambaza jumla ya vyandarua vyenye dawa milioni 17.6 bila malipo katika kaya, katika mikoa yote ya Tanzania Bara,” alisema waziri.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment