Home » » Spika wa Bunge awataka Wabunge kuchangia bajeti na si kupigana vijembe

Spika wa Bunge awataka Wabunge kuchangia bajeti na si kupigana vijembe


SPIKA wa Bunge Anne Makinda amewataka wabunge warudishe heshima ya Bunge kwa kuacha tabia za kupigana vijembe wakati wanapochangia Bajeti ya Serikali.

Makinda amesema michango ya wabunge ni muhimu katika kuboresha Bajeti ya Serikali, hivyo kama wakiacha kuchangia na kuingia kwenye malumbano ya kisiasa, hawawezi kuisaidia Serikali na wananchi waliowatuma.

Makinda alitoa mwito huo jana baada ya kipindi cha maswali na majibu baada ya siku mbili za mjadala wa bajeti hiyo kutawaliwa na malumbano ya kisiasa hali iliyowalazimisha wabunge kutoa lugha za kuudhi.

Spika huyo alisema amepokea simu nyingi zinazowashutumu wabunge kuhusu hali iliyojitokeza katika mjadala wa bajeti kuanzia Jumatatu.

“Nimepokea simu wananchi wanasema wabunge hamjadili bajeti ila mnachofanya hapa mnalumbana,” alisema Makinda.

Alisema wabunge wakiendelea kuonesha ubingwa wao wa kupiga siasa katika kujadili bajeti hiyo, wananchi waliowatuma watasikitishwa na hali hiyo.

Alisema ushauri wa wabunge ni muhimu ili Serikali ijue iboreshe wapi na ipunguze wapi matumizi ili wananchi wapatiwe bajeti nzuri.

“Wananchi wanawaona mmoja mmoja mnayofanya hapa, nawaombeni mrudishe heshima ya Bunge,” alisema Makinda.

Kiongozi huyo pia aliwaka wabunge hao wajihurumie wenyewe kwa mambo ya ajabu wanayofanya ukumbini ya kuonesha ubingwa wa kupiga siasa.

Akiahirisha Bunge baada kumalizika kwa kipindi cha asubuhi, Spika Makinda alieleza kuridhishwa na michango ya wabunge waliochangia kuanzia asubuhi.

Waliochangia asubuhi, walikuwa wabunge 15 ambao ni Yussuf Nassir (Korogwe Mjini –CCM); Salvatory Machemli (Ukerewe – Chadema); Henry Shekifu (Lushoto – CCM); Luhaga Mpina (Kisesa – CCM); Dk Kebwe Stephen (Serengeti – CCM); Albert Ntabaliba (Manyovu – CCM); Desderius Mipata (Nkasi Kusini – CCM) na Danstan Kitandula (Mkinga – CCM).

Wengine ni Meshack Opulukwa (Meatu –Chadema); Kidawa Himid Saleh (Viti Maalumu – CCM); Dk Titus Kamani (Busega – CCM); Mariam Kisangi (Viti Maalumu – CCM); Augustino Masele (Mbogwe – CCM) na Masoud Abdalla Salum (Mtambile – CUF).

Wakati huo huo, Makinda alisema Muswada wa Sheria ya Fedha ambao awali ulipangwa kupitishwa kesho baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Serikali, sasa utasubiri hadi mwishoni mwa Mkutano wa Nane wa Bunge.

Spika alisema wamefanya hivyo baada ya utafiti kubaini kuwa mabunge mengi ya Jumuiya ya Madola yana utaratibu wa kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha na Muswada wa Sheria ya Matumizi mwishoni kabisa mwa mjadala wa bajeti.

Alisema kwa kuzingatia ombi la Serikali na wabunge walio wengi pamoja na maoni ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, muswada huo sasa utapitishwa mwishoni mwa mkutano unaoendelea kwani bado Serikali inaweza kukusanya mapato kabla ya muswada huo kupitishwa.

Kutokana na mabadiliko hayo, Makinda alisema sasa mjadala wa bajeti utakuwa wa siku tano badala ya nne na hivyo utahitimishwa kesho Ijumaa.
Chanzo: Michuzi Blog

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa