Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WABUNGE wameitaka Serikali iharakishe Muswada wa Haki ya Kupata Habari na Muswada wa Huduma za Vyombo vya Habari.
Ushauri huo ulitolewa bungeni jana, wakati wabunge walipochangia bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, iliyowasilishwa na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Fenela Mukangara.
Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM), alisema miswada hiyo ni muhimu, kwa kuwa itasaidia kuendeleza sekta ya habari nchini.
“Miswada hii ikikamilika itatuwezesha kupatikana kwa sheria zitakazosimamia tasnia ya habari nchini na kuifanya iendeshwe kwa kuzingatia taaluma, weledi, miiko na maadili.
“Pia itatoa fursa kwa umma kupata taarifa zinazowahusu, kwa kuwa jambo hili ni haki yao ya msingi kama inavyotamkwa katika ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania,” alisema Nkamia.
Alisema kamati yake inashauri Serikali iendelee kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) pamoja na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa ajili ya kuhakikisha wadau sekta ya habari wanatimiza wajibu wao.
Naye, Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika wizara hiyo, Joseph Mbilinyi, alisema Kambi ya Upinzani inataka kauli ya Serikali kuhusu mchakato wa uwapo wa sheria hiyo.
Kuhusu Sheria ya Kulinda Chanzo cha Habari, Mbilinyi alisema taarifa muhimu ambazo kwa kiasi kikubwa zinahusu matumizi ya rasilimali za nchi, zimekuwa zikifanywa siri na hivyo kuwanyima wananchi haki ya kuzifahamu.
Awali, akisoma hotuba ya bajeti hiyo, Dk. Mukangara, alisema waraka wa mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari umekamilika na kuwasilishwa katika ngazi ya juu kwa uamuzi wa Serikali na hatimaye bungeni katika kipindi cha mwaka huu wa fedha 2012/2013.
Aidha, alisema kutungwa kwa sheria hiyo kutaimarisha weledi na uwajibikaji wa vyombo vya habari hapa nchini.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment