Home » » BALOZI SEIF KUZINDUA MAONYESHO YA NANENANE

BALOZI SEIF KUZINDUA MAONYESHO YA NANENANE



Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SIKUKUU ya Wakulima ya Nanenane kwa mwaka 2012, inatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Nzuguni, mkoani Dodoma.


Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mbogo

Futakamba, ilisema sherehe hizo zimelenga zaidi kuonyesha mafanikio na changamoto za sekta ya kilimo, yakihusisha wadau wote kuanzia Kijiji hadi Taifa. 

Maonyesho hayo hufanyika pia kikanda katika Viwanja vya John Mwakangale, eneo la Uyole, Mbeya, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Themi Arusha, Kanda ya Kaskazini, Uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Manispaa ya Morogoro, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Ziwa, Viwanja vya Nyamhongolo, mkoani Mwanza na Kanda ya Kusini, viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

Taarifa hiyo ilisema washiriki wakubwa ni wadau wa sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, ushirika, wajasiriamali, wizara, tasisi za serikali, sekta binafsi na wajasiriamali.

Aidha, taarifa hiyo ilisema sherehe za Nanenane huandaliwa na kuratibiwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika pamoja Chama cha Wakulima Tanzania (TASO).

Mgeni rasmi katika ufunguzi huo, anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Iddi.

Taarifa hiyo ilisema sherehe hizo, zinatarajiwa kufungwa na Rais Jakaya Kikwete.

Kaulimbiu ya Nanenane mwaka huu ni “Kilimo Kwanza–Zalisha Kisayansi na Kiteknolojia Kukidhi Mahitaji ya Ongezeko la Idadi ya Watu.”

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa