JIBU LA SWALI LA MBUNGE Same mashariki
na Mwandishi wetu, Dodoma
SERIKALI imezitaka taasisi zake zote hapa nchini kuutangaza Mlima Kilimanjaro kutokana na kuwa maarufu duniani kote.
Wito huo ulitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM).
Nyalandu alisema mlima huo ni maarufu sana duniani ndiyo maana awali nchi ya Kenya ilikuwa ikisema uko kwao hadi Tanzania ilipoamua kufuatilia suala hilo.
Katika swali lake, Kilango alitaka kujua kauli ya serikali kuhusiana na uongo ambao umekuwa ukitumika kuwa Mlima Kilimanjaro uko nchini Kenya.
Katika swali la msingi, mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (CHADEMA), alitaka kujua kauli ya serikali juu ya mkanganyiko uliopo kutokana na Wakenya kuutangaza Mlima Kilimanjaro kuwa uko Kenya na serikali ya Tanzania inatangaza Mlima huo uko Tanzania.
Katika jibu lake, Nyalandu alisema umaarufu wa mlima huo katika soko la utalii duniani ni kubwa na wenye kuvuta hisia za wadau wa utalii, wapenzi na wapanda milima kote ulimwenguni na hivyo imesababisha mvutano ulipo mlima huo na mji gani wageni wapite.
Alisema ili mtu aweze kupanda Mlima Kilimanjaro ni sharti afike Mkoa wa Kilimanjaro na kupanda mlima kupitia njia zake rasmi za Marangu, Machame, Lodorosi, Umbwe na Rongai ambazo husimamiwa na Shirka la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment