Home » » MALAWI YADAI ZIWA NYASA NI MALI YAKE

MALAWI YADAI ZIWA NYASA NI MALI YAKE

Na Maregesi Paul, Dodoma
SERIKALI ya Malawi, imetangaza kwamba Ziwa Nyasa ni mali ya nchi hiyo. Taarifa hiyo ilitolewa bungeni na Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), baada ya kuomba Mwongozo wa Spika dakika chache kabla ya Bunge kuahirishwa jana mchana.

Kwa mujibu wa Zambi, Malawi imetoa tangazo hilo kupitia Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo na Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa nchi hiyo, ambaye hakumtaja jina.


“Mheshimiwa Mwenyekiti, gazeti la Kiingereza la kila siku linalomilikiwa na Serikali yetu, juzi liliandika kwamba, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi, ametangaza kuwa Ziwa Nyasa lote ni mali ya nchi ya Malawi.


“Katibu huyo anasema wao wanatumia sheria ya mwaka 1890 iliyotungwa na Wajerumani, ambayo alisema inaonyesha Ziwa Nyasa lote ni la Malawi.


“Mheshimiwa Mwenyekiti, tangazo hilo limewatia hofu wananchi wa Mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, kwa hiyo, naomba mwongozo wako juu ya jambo hili kwa sababu lina utata,” alisema Zambi.


Akijibu mwongozo huo, Kaimu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, alisema Tanzania iko tayari kwa lolote pindi itakapochokozwa.


“Kwanza kabisa, napenda kusema kuwa, Serikali imesikitishwa na kauli ya huyo Katibu wa wizara moja huko Malawi, kwa sababu sisi tunajua mazungumzo ya huo mpaka bado yanaendelea.


“Lakini, Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwatoe hofu wananchi wa Mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, kwamba waendelee na shughuli zao bila wasiwasi katika ziwa hilo.


“Serikali yetu imekaa vizuri, tuko tayari kwa uchokozi wowote, sisi tunafuata sheria za kimataifa, nawaambia wananchi tumesimama vizuri wasiwe na wasiwasi kabisa.


“Hata hivyo, taarifa kamili itatolewa Jumatatu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,” alisema Sitta na kupigiwa makofi.


Wakati huo huo, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema kuanzia Septemba mosi, mwaka huu, ni marukufu mabasi ya abiria kusimama porini kwa ajili ya abiria kujisaidia.


Dk. Mwakyembe alitoa agizo hilo jana, alipokuwa akihitimisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, aliyoiwasilisha bungeni juzi.


“Kwa mila zetu ni aibu kuona mwili wa mama, lakini utashangaa abiria wanapokuwa safarini, mabasi yanasimama na abiria kuchimba dawa wakiwa karibu karibu.


“Huu siyo utaratibu wetu na siyo mila zetu, kwa hiyo, kuanzia Septemba mosi mwaka huu, basi lolote la abiria litakalosimama porini ili abiria wachimbe dawa, kwanza litapewa onyo, likikamatwa tena litatozwa faini na likikamatwa kwa mara nyingine, litafutiwa leseni ya biashara.


“Hili litasimamiwa na lazima litekelezwe, tutawakamata na atakayelalamika aende mahakamani, nendeni mahakamani na nitawashinda,” alisema Dk. Mwakyembe huku wabunge wengi wakimpinga
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa