Home » » SERIKALI YATAKIWA KUIMARISHA UCHUMI

SERIKALI YATAKIWA KUIMARISHA UCHUMI


na Danson Kaijage, Dodoma
SERIKALI imetakiwa kuweka mfumo mzuri wa kiuchumi ambao utawanufaisha Watanzania wote, vinginevyo taifa litazidi kuwa na watu maskini.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Padri wa Kanisa Kuu Katoliki Jimbo la Dodoma, alipokuwa akihubiri katika ibada ya utangulizi wa ufunguzi wa mahafali ya tatu ya darasa la saba katika Shule ya Msingi ya St. Ignatius iliyopo mjini hapa.
Padri Lali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Askofu Mkuu wa kanisa hilo alisema kuwa serikali inatakiwa kuhakikisha inaweka mfumo mzuri wa kiuchumi ambao utawawezesha Watanzania wote kuondokana na umaskini ambao kwa sasa ndiyo wimbo wa Watanzania walio wengi.
Alisema  pamoja na taifa kuwa na rasilimali nyingi lakini kutokana na mfumo mbovu wa uchumi uliopo imesababisha Watanzania kuwa maskini kutokana na kushindwa kufaidi rasilimali zilizopo.
“Mfumo huu mbovu uliopo unawasababishia watanzani wengi kuendelea kuwa maskini, na hali hii ni hatari sana kwa vizazi vijavyo, kwani tutalaumiwa na kizazi cha baadaye watakapoona kuwa nchi ilikuwa na rasilimali za kutosha lakini zinafaidiwa na wachache.
“Ili kuondokana na hili na kuwafanya Watanzania kuishi maisha mazuri na ya furaha na amani ni lazima kuwepo mfumo wa kiuchumi ambao utakuwa na fursa sawa kwa Watanzania wote kufaidika na kile kinachopatikana na wala si Watanzania wachache wanufaike huku walio wengi wanaendelea kuimba wimbo wa umaskini,” alisema Padri Lali.
Aidha, kiongozi huyo wa kiroho aliwataka wazazi kuwalea watoto wao katika misingi bora ya uadilifu ili kuwafanya watoto wao kutojihusisha na vitendo vya kifisadi pindi wapatapo kazi mahali popote.
“Kinachosababisha kuwepo kwa viongozi mafisadi katika vitengo mbalimbali serikalini na katika taasisi mbalimbali ni kutokana na viongozi hao kutokuwa na hofu ya Mungu, jambo ambalo linawafanya kujipenda wao bila kuwafikiria wenzao,” alisema Padri Lali.
Aliwaasa pia wazazi kuwa karibu na watoto wao ili waweze kukaa nao kwa malengo ya kubadilishana nao mawazo kwa lengo la kujua mawazo ya watoto wao wanayoyafikiria.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa