Home » » WANANCHI WAZUIA UJENZI WA DARAJA

WANANCHI WAZUIA UJENZI WA DARAJA


na Danson Kaijage, Mtera
WANANCHI kutoka familia 18 za Kijiji cha Mloda, Kata ya Makang’wa, Jimbo la Mtera wilayani Chamwino, Dodoma wakishirikiana na mbunge wao, Livingstone Lusinde (CCM), wamekwamisha ujenzi wa daraja katika barabara kuu ya Dodoma-Iringa kwa kushinikiza walipwe fidia ya sh milioni 52.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana, wananchi hao walisema hawapo tayari kuruhusu ujenzi kuendelea hadi Wakala wa Barabara (Tanroad) Mkoa wa Dodoma, atakapowalipa fidia yao ambayo inatokana na kuachia nyumba zao pamoja na mashamba kama walivyoahidiwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi hao; Peter Mhina, Mauta Milimo, Pauli Kumunda na George Kumunda, walisema tangu ujenzi huo uanze karibu mwaka mmoja na nusu sasa, hawajui hatma yao ya kulipwa fidia.
Walisema kutokana na ucheleweshaji huo, hawana sehemu ya kuishi na mashamba yao ambayo yalikuwa yakiwaingizia kipato hayapo, hivyo kuendelea kuishi maisha ya shida na dhiki.
“Hatuwezi kuendelea kuishi kwa shida kiasi hiki wakati tulikuwa na mali zetu, sio kwamba tunakataa maendeleo ya nchi, lakini hatukubali ubabaishaji unaofanywa na serikali.
“Hatujui hatma ya maisha yetu tuliambiwa tutalipwa fidia, hadi leo hatujui kinachoendelea,” alisema mmoja wa wanafamilia hao.
Mbali ya hilo, wakazi hao wameushutumu uongozi wa kijiji hicho kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa Tanroad kuwazunguka na kukwamisha ulipwaji wa fidia hiyo.
Naye mbunge wa eneo hilo, Lusinde, alisema anaungana na wanafamilia hao kutopisha ujenzi wa daraja, kwani ni haki yao kulipwa fidia.
“Mimi kama Mbunge wa Mtera na hao wananchi wakiwa ni wapigakura wangu, ninachosema kutoka moyoni, naungana nao kuzuia ujenzi wa daraja mpaka watakapolipwa fidia wanazozidai,” alisema.
Alipotafutwa Meneja wa Tanroad Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, alikiri kuwapo kwa familia zinazodai fidia na kuzitaka kuwa na subira kwani serikali inashughulikia malipo hayo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa