na Happiness Mtweve, Dodoma
JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dodoma umekiri kutafunwa na kuumizwa na makundi ya kisiasa yaliyomo ndani ya chama hicho.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Dodoma ambaye pia ni wakili wa kujitegemea, Anthony Mavunde, akifungua kikao cha Baraza Kuu la UVCCM Mkoa wa Dodoma.
Mavunde alisema makundi hayo mengi huwa yanaanzia zinapofika nyakati za uchaguzi kutokana na watu kutokutaka ushindani wa kisiasa na badala yake hujikuta wakieneza chuki na kuibua makundi.
Alisema imefika wakati vijana wanaonesha msimamo na kutokukubali kutumiwa na makundi hayo ambayo huwatumia wakati wa uchaguzi na unapokwisha ujamaa na urafiki wao huishia hapo na hata wakipigiwa simu hugoma kupokea na kueneza kuwa wanaombwa pesa.
“Tupo tayari kutumiwa na vijana wenzetu kwa masilahi ya jumuiya na si kwa masilahi ya watu binafsi ambao hawakubali kupingwa kwa ajili ya manufaa kwa ajili ya kutimiza malengo yao.
“Tujifunze kutokujenga chuki na uhasama na kuacha kulazimisha nafasi za uongozi na siasa, si kujengeana chuki, ushindani hauepukiki kwenye siasa hivyo chuki hizo zinapaswa kuishia wakati wa uchaguzi na unapokwisha warudishe umoja na wajenge jumuiya yao,” alisema Mavunde.
Alisema makundi ya siasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi yamekuwa yakiwaaumiza sana vijana kwani amewaomba vijana wenzake kutokubali kutumiwa na watu wengine kwa ajili ya kutimiza malengo yao binafsi ya kisiasa.
Alifafanua kuwa kumekuwa na mashinikizo ya watu wanaopenda kutumia vijana kwa malengo yao ya kisiasa na kwamba ufike wakati na wao wajitambue.
Mavunde alisema kukubali kuendelea kutumiwa ni kukiua chama ambacho kinawategemea vijana kwa kiasi kikubwa na kwamba kuanzia leo wasiwe tayari kutumiwa na wanasiasa kwa masilahi yao binasfi, bali wawe tayari kutumiwa na vijana wenyewe.
Alieleza kuwa kupishana kisiasa si maana ya kuchukiana bali huenda kuna maana nyingine kuwa hukutosha, lakini yote hayo yaishie kwenye uchaguzi na ukiisha wawe kitu kimoja.
Mavunde alitumia fursa hiyo kuwashukuru watendaji wote wa UVCCM mkoa kwa ushirikiano waliutoa hadi kusababisha mafanikio yaliyopatikana na kusema yeye binafsi hajawahi kuhitilafiana kwa ugomvi mkubwa bali walikuwa wanatofautiana kwa hoja tu.
Kwa wale wote waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali amesema atawaunga mkono kwa kila hali kwani CCM imara inabebwa na vijana na kuwataka kuwa wajasiri na wenye imani ili waweze kufanikiwa.
Akielezea mafanikio aliyoyapata katika uongozi wake alisema mbali na kufanikisha uendelezaji wa miradi mbalimbali lakini pia amefanikisha umoja, mshikamano na usawa miongoni mwa wana UVCCM kama alivyoahidi wakati anaomba nafasi ya uenyekiti wa mkoa na kusema hilo amelifanya kwa kuweka fursa sawa na vijana wote kuonekana wamoja.
Mavunde aliwaomba viongozi wajao kutilia msisitizo katika uanzishaji wa SACCOS kwa vijana katika maeneo yao kama walivyowahi kukubaliana katika vikao ili waweze kuwakwamua vijana kiuchumi.
Aidha, aliwataka viongozi kutumia nafasi zao kushiriki na kuhamasisha vijana kushiriki katika zoezi la sensa ili kuipa serikali takwimu sahihi ya watu wake na kuweza kupanga mipango yake vizuri.
Kwa upande wake Katibu wa CCM mkoa, Albert Mgumba, amewataka kuchagua viongozi imara watakaokiletea chama ushindi na watakaopambana na hali ya sasa ya siasa ya vyama vingi na wala wasiangalie kiongozi anayetaka kuchaguliwa kwa fedha.
Alisema kutokana na mabadiliko ya nchi wanataka kupata viongozi wazuri na kuwataka wote watakaochaguliwa kipindi hiki wajue kuwa wamechaguliwa kupambana na hali ya sasa ilivyo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment