na Tamali Vullu, Dodoma
WANAFUNZI 20 waliofanya vizuri katika mitihani yao ya kumaliza kidato cha sita mwaka huu wamepongezwa na Bunge pamoja na kukabidhiwa zawadi mbalimbali, ikiwamo fedha taslimu sh 200,000 kila mmoja.
Hafla ya kuwapongeza wanafunzi hao kutoka shule nane za serikali na mbili za binafsi ilifanyika bungeni jana baada ya Bunge kutengua kanuni na kuruhusu wanafunzi hao kuingia ukumbini.
Mbali na fedha taslimu, wanafunzi hao walipewa zawadi za kompyuta ndogo (Laptop) na cheti ambavyo walikabidhiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Pia kila shule iliyotoa mwanafunzi au wanafunzi bora imezawadiwa sh milioni moja.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema jana kuwa hafla hiyo inafanyika ili kuwaenzi na kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri.
Alisema kati ya wanafunzi 44,160 waliofanya mtihani huo mwaka huu, 40,775 walifaulu ambao ni sawa na asilimia 92.2.
Waziri huyo alisema kuwa kati ya waliofaulu, waliopata kiwango cha daraja la kwanza hadi la tatu ni 35,201.
Alisema vijana hao wanapongezwam, ili kuwatia moyo na kuongeza hamasa kwa wengine waliopo shuleni.
Aliwataja wanafunzi hao na shule zao kuwa ni Faith Assenga, Immaculata Mosha, Rachel Sigwajo, Mary Kiangi, Nashivai Kivuyo, Evelyine Mapunga na Neema Munuo, wote kutoka shule ya Marian ambao walikuwa wakichukua masomo ya mchepuo wa sayansi (PCM).
Wengine ni Neema Kiula (Kilakala), Ester Marcel (Ufundi Ifunda), Prisca Longo (Tabora wasichana), Zawadi Mdoe na Jamal Juma (Feza), Belinadino Mgimba (Minaki), Gwamaka Njobelo, Nickson Mwamsojo na Benson Maruchu (Mzumbe).
Wengine ni Faridi Abdallah (Mpwapwa), Alex Isdor na Julius Luvanda (Kibaha) na Brighton Lema (Tabora wavulana).
Akizungumza kabla ya kuwakabidhi zawadi hizo, Waziri Mkuu, Pinda, aliwasihi wanafunzi hao kutumia vizuri fursa watakapokuwa vyuoni, kwani huko kuna utawala binafsi zaidi tofauti na shule za sekondari.
Naye Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliwasihi vijana hao kujiepusha na makundi mabaya ambayo yataweza kuzoretesha maendeleo yao katika masomo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment