na Tamali Vullu, Dodoma
CHAMA cha Skauti Tanzania kimekumbwa na kashfa baada ya viongozi wake kudaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Kashfa hiyo iliibuliwa bungeni jana na Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (CHADEMA), alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Alisema viongozi wa chama hicho wameacha kutekeleza majukumu yao ya msingi, na badala yake yamekuwa wakijinufaisha wao binafsi.
“…Siku za hivi karibuni, viongozi wa Skauti wamekuwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuacha majukumu ya msingi, jambo hili ni hatari katika mustakabali wa nchi yetu.
“Viongozi hawa wamefikia hatua ya kuwasafirisha watu nje ya nchi ambao si walengwa ili waweze kufanikisha mambo yao,” alisema na kuongeza kuwa, watu wengi wanaopelekwa nje ya nchi ni wafanyabiashara wenye mtandao wa dawa za kulevya.
Alisema wakati wa Jubilee ya Malkia wa Uingereza, viongozi wa chama hicho waliwapeleka watu wasiohusika kabisa katika chama hicho (sio Skauti) ambao wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Aidha, alisema Mkurugenzi wa shule moja (hakumtaja jina) alitoa sh milioni 45 kwa ajili ya wanafunzi wa shule yake wapelekwe nje ya nchi, lakini hicho hakikufanyika na mpaka sasa amelipwa sh milioni 28 na bado anaendelea kukidai chama hicho.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, aliitaka serikali kusoma alama za nyakati kwa kutatua kero mbalimbali za watumishi wake wakiwamo walimu.
Pamoja na hilo, aliitaka serikali kuwarudisha masomoni wanafunzi 25 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kusema kuwa endapo Mwalimu Julius Nyerere angekuwa anatumia ubabe, Samwel Sitta (Waziri wa Afrika Mashariki), leo hii asingekuwa na wadhifa huo.
Naye mbunge wa Viti Maalumu, Betty Machangu, aliishauri serikali kuondoa utaratibu wa maswali ya kuchagua kwa wanafunzi ili kuwawezesha kutumia akili zao.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment