Home » » WAZIRI: KAZI YA MAHAKAMA NI KUSIMAMIA HAKI, SI VIFUNGO

WAZIRI: KAZI YA MAHAKAMA NI KUSIMAMIA HAKI, SI VIFUNGO


na Happiness Mtweve, Dodoma
WATANZANIA kote nchini wametakiwa kutambua kuwa kazi ya mahakama si kutoa vifungo jela kama wengi wanavyodhani, bali ni chombo kilichoanzishwa  kwa ajili ya kutoa na kusimamamia haki kwa kila raia pasipo kujali hadhi wala itikadi.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea mahakama zilizopo katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
“Mahakama haipo kwa ajili ya kuwapeleka watu jela tu kama wananchi wengi hasa vijijini wanavyofikiri, bali ni chombo kinachowawezesha raia kupata haki zao hivyo wasiogope bali waitumie,” alisema Kairuki.
Vile vile Kairuki aliwaasa wananchi kujitolea kujenga majengo ya mahakama endapo ya zamani yatakuwa yamechakaa, katika maeneo ambayo yana uhitaji huo.
Kwa upande mwingine aliwaonya mahakimu na watendaji wanaoendekeza rushwa kuacha tabia hiyo, kwa kuwa wanakosesha wengine kupata haki zao.
“Nimetembelea katika Gereza la Isanga nimekuta watu sita wamehukumiwa miaka minane, sasa bila kupatiwa nakala za hukumu, haiwezekani kutoa hukumu bila ya nakala, ni kosa, kwani ni haki ya mtu kukata rufaa anapoona ama kuhisi ameonewa, hivyo asipokuwa na nakala atashindwa kufanya hivyo,” alisema Kairuki.
Baadhi ya changamoto alizozibaini kairuki katika ziara hiyo ni pamoja na upungufu wa mahakimu, ukosefu wa vitendea kazi na uchakavu mkubwa wa majengo katika baadhi ya mahakama za mwanzo zilizopo katika wilaya hiyo.
Katika ziara hiyo, Kairuki alibaini kuwa kati ya mahakama 10, nne ndizo zinazofanya kazi, zilizobakia hazifanyi kazi kutokana na ukosefu wa mahakimu na changamoto za usafiri.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa