HOFU ya kutochaguliwa katika uchaguzi ujao
imemfanya Diwani wa Kata ya Msisi, Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, Chunga
Mgalilwa (CCM), ashindwe kuwazuia wananchi kukata na kuchoma Msitu wa Goima.
Diwani huyo alitoa kauli hiyo jana wilayani humo
katika kikao cha Baraza la Madiwani wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji
wa shughuli za kata yake kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha
2012/2013 (Julai hadi Septemba 2013).
Hatua ya Mgalilwa kutoa kauli hiyo ilitokana na
tuhuma alizopewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Betty Mkwasa, kuwa anahusika
kuhamasisha wananchi kutumia msitu huo kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwamo
uchomaji wa mkaa na ukataji wa kuni.
Pia diwani huyo anashutumiwa kuwa kiongozi katika
kamati ya watu watatu aliyoiunda na madiwani wenzake kwa lengo la kuzuia
jitihada za serikali kuzuia uharibifu wa mazingira katika msitu huo.
Akijibu tuhuma hizo, Mgalilwa alikiri kuhusika
katika kamati hiyo na kuongeza kuwa yeye si mwenyekiti wa kamati bali ni mjumbe
na hawezi kuwakataza wananchi kutotumia msitu huo kwani katika uchaguzi ujao
anaweza kukosa kura, kwakuwa wananchi hao ndio anaowategemea kumpa ushindi.
“Wananchi wa kijiji hiki wamekuwa wakitumia msitu
huu kwa kipindi kirefu bila kuingiliwa na serikali, jambo ambalo
nashangaa ni kwanini serikali imeona umuhimu wa msitu huo kwa kipindi cha hivi
karibuni na kuwataka wananchi waache kuutumia msitu huo,” alisema.
Hata hivyo, Mkwasa alimtaka diwani huyo kutoa
ushirikiano kwa serikali katika kukabiliana na wavamizi hao, kwakuwa siku za
hivi karibuni serikali ya wilaya ilipima mipaka katika msitu huo pamoja na
kuweka matangazo ya kuzuia shughuli mbalimbali lakini wananchi walitoa mabango
hayo ya matangazo na kuendelea na ukataji wa miti.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment