TUHUMA za ujangili na Operesheni Tokomeza UIjangili
inayoendeshwa na serikali, jana ziliiteka Bunge baada ya Mbunge wa Mwibara,
Kangi Lugola (CCM), kuituhumu serikali kwa kutoa hoja nyepesi bungeni.
Lugola alisema operesheni hiyo inafanyika kwa
kukiuka haki za binadamu, kwamba watu wasiokuwa majangili wamekamatwa, kuteswa
na kuharibiwa mali zao ilhali majangili wanaojulikana wakiachwa waendelee na
uhalifu wao.
Wakati mbunge huyo akitoa tuhuma hizo, Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, aliwatuhumu wabunge na
wanasiasa wengine kwa kuingilia utendaji wa operesheni hiyo kwa kuwatetea
wanaokamatwa kwa kujihusisha na ujangili.
Kauli ya Nahodha ilionekana kumpiga kijembe Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambaye
wiki iliyopita msaidizi wake (ofisi ya ubunge) alikamatwa mkoani Iringa kwa
tuhuma za ujangili.
Jana Lukuvi alidai anao ushahidi ‘mzito’ wa mateso
aliyoyapata msaidizi wa ofisi yake, ambaye aliachiwa juzi baada ya kuonekana
kutohusika na ujangili kama ilivyokuwa ikidhaniwa.
Hoja ilivyoanza
Hoja hiyo ilitokana na swali la nyongeza
lililoulizwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), aliyetaka kujua kwanini
serikali inaendelea kuwalinda wanasiasa, askari na watendaji wake
wanaojihusisha na ujangili.
Lembeli pia alitaka kujua kwanini serikali
haiwachukulii hatua za kisheria makamanda wa polisi wa mipakani, hasa wale
wanaopakana na mbuga ya Serengeti, wanaojihusisha na ujangili, kutorosha nyara
za serikali pamoja na kushirikiana na majangili.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na
Mazingira, Lazaro Nyalandu, alisema kamwe wizara yake haiwalindi wanasiasa,
wabunge, maofisa wa polisi na watendaji wa serikali wanaohusika na ujangili.
Nyalandu alisema kuanzia sasa kila kiongozi
atakayekamatwa kwa tuhuma za ujangili atatangazwa hadharani.
Alisema si sahihi kuwatuhumu wabunge, polisi na
watendaji wengine wa serikali bila ya kuwa na utafiti juu ya tuhuma zao.
Hoja ya Lugola
Mara baada ya kipindi cha maswali na majibu
kumalizika, Lugola aliomba mwongozo wa spika akitumia kanuni ya Bunge ya 67,
ambapo alilitaka Bunge liiagize serikali kutoa taarifa ya operesheni hiyo
inayofanyika nchi nzima.
Lugola aliomba mwongozo huo akisema kuwa majibu ya
Waziri Nahodha na Nyalandu juu ya suala hilo ni ya mzaha mzaha yenye lengo la
kuendeleza kulindana.
Mbunge huyo alilitaka Bunge liilazimishe serikali
kutoa taarifa rasmi juu ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Mara baada ya Lugola, kuzungumza alisimama Lukuvi
ambaye alitaka serikali iachwe imalize operesheni hiyo bila kutoa taarifa kwani
wakifanya hivyo wanaweza kusababisha wahusika wakimbie au kupoteza ushahidi.
Alisema taarifa za operesheni hiyo
zitapelekwa katika kamati zinazohusika mara baada ya kufikia tamati na baadae
zitafikishwa bungeni kulingana na taratibu zinazotakiwa.
Lukuvi pia alionyesha simu yake ya mkononi akidai
ina ushahidi wa mateso yanayofanywa dhidi ya wanaokamatwa kwa tuhuma za
ujangili.
“Nina ushahidi wa msaidizi wangu alivyoteswa baada
ya kukamatwa kuwa ni jangili, huyu wamemuachia jana, nawaombeni tuache operesheni
hii imalizike ndipo tupatiwe taarifa zake,” alisema.
Naibu Spika Job Ndugai, aliunga mkono kauli ya
Lukuvi akidai taarifa za operesheni hiyo zikitolewa sasa zitaharibu zoezi hilo.
Hoja ya Lema
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amesema
anatarajia kuwasilisha maelezo binafsi bungeni kuitaka serikali izuie uwindaji
wa tembo katika vitalu vilivyo karibu na hifadhi au mbuga.
Lema alisema ameamua kufanya hivyo kutokana na
ujangili kuzidi kushika kasi. Inakadiriwa tembo 30 wanauawa kila siku.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment