Baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Vijana wa CCM
(UVCCM), wameanza kupanga upya mikakati ya kuwang’oa viongozi wa juu wa jumuiya
hiyo baada ya kushindwa kwa mpango uliokuwa umepangwa kutekelezwa wakati wa
kikao cha baraza hilo kilichofanyika juzi mjini Dodoma.
Wanamapinduzi walikuwa wamepanga kuwatoa madarakani Mwenyekiti wa
UVCCM, Sadifa Juma Khamis na makamu wake, Mboni Muhita, lakini jaribio hilo
lilishindwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni wahusika
kutojipanga vizuri, pia uwapo wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana katika
mkutano huo.
Kinana anatajwa kukwamisha mapinduzi yaliyokusudiwa kutokana na
kauli yake aliyoitoa wakati akifungua mkutano huo kwamba haukuwa kwa ajili ya
kuibomoa jumuiya bali kuijenga, hali ambayo iliwafanya wajumbe waliokuwa na
ajenda ya kumng’oa mwenyekiti kunywea.
Hata hivyo, jana gazeti hili lilielezwa kuwa baadhi ya
wajumbehawakuridhika na hatua ya kutokujadiliwa kwa hali ilivyo ndani ya UVCCM,
hivyo wameamua kujipanga upya ili kutekeleza azma yao ya kuwasulubu viongozi
wao katika mkutano ujao.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho alisema kumekuwa na woga
unaowafanya viongozi wa juu wa UVCCM kutoruhusu kuwapo kwa ajenda zaidi ya moja
katika vikao vya Baraza Kuu na kwamba huo ni utumiaji mbovu wa rasilimali za
jumuiya.
“Kikao kimoja cha baraza kinagharimu zaidi ya Sh60 milioni, lakini
mwaka huu pekee tumefanya vikao vitatu kwa hiyo tumetumia zaidi ya Sh180
milioni. Fedha hizi zingeweza kugharimia mambo mengine kama uhaba wa kadi na
kanuni za jumuiya kwenye ngazi za chini,” alisema mmoja wa wajumbe kutoka mikoa
ya Kanda ya Kati, huku akiomba jina lake lihifadhiwe.
Alisema kwa mujibu wa kanuni za jumuiya hiyo, kikao cha Baraza Kuu
kinapaswa kuwa kimoja kwa mwaka, lakini mwaka huu tayari wamefanya vikao vitatu
ambavyo kimsingi havina tija kwani hakuna kilichojadiliwa kutokana na woga wa
viongozi.
Mjumbe mwingine kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini alisema jumuiya
imeshindwa kuteua makamanda wa wilaya na mikoa kwa muda mrefu, pia kutofanya
uteuzi wa wagombea wa nafasi za chipukizi katika ngazi za wilaya na mikoa.
“Mwakani tunakabiliwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini cha
ajabu hadi sasa tuna viporo vingi, mikutano kama hii ingetumika kufanya kazi
hizo badala ya kujadili ajenda moja tu kama tulivyofanya Zanzibar mwezi
uliopita na jana (juzi) hapa Dodoma,” alisema.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda akijibu hoja hiyo
alisema: “Uhai wa jumuiya ni vikao, kwa hiyo siyo kosa kufanya vikao hata kama
vitakuwa ni zaidi ya 10 kwa sababu katika vikao ndiko mambo muhimu
yanakojadiliwa”.
Kuhusu uteuzi wa makamanda wa vijana wa wilaya na mikoa, Mapunda
alisema kazi hiyo ilifanyika na kukamilika juzi katika kikao cha Kamati ya
Utekelezaji cha jumuiya hiyo na kwamba suala la wagombea wa chipukizi nalo
litakamilishwa.
CHANZO: TANZANIA
DAIMA
0 comments:
Post a Comment