Spika
wa Bunge, Anne Makinda amesema hatishwi na mchakato wa kumng’oa katika
nafasi yake ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla
kutokana na tuhuma za kukiuka kanuni za Bunge.
Kadhalika
Spika Makinda amepuuza hoja za Dk Kigwangalla akisema kuwa yeye
hajavunja kanuni yoyote, lakini akaweka bayana kuwa mbunge huyo wa Nzega
ana haki kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kuendelea na kile anachokifanya.
“Kanuni
si zinamruhusu, utaratibu upo kwenye kanuni za Bunge kwa hiyo aendelee
na mchakato lakini mimi ninachosema sitetereki maana hakuna kanuni
yoyote ambayo nimeivunja,” alisema Makinda katika mahojiano maalumu na
Mwananchi ofisini kwake jana.
Wakati
Spika akitoa kauli hiyo, jana, Dk Kigwangalla alianza harakati zake za
kukusanya saini za wabunge, akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya
kutokuwa na imani naye kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni.
Miongoni
mwa madai ya Dk Kigwangalla ni hatua ya Makinda kufanya uteuzi wa
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Bajeti, tofauti na kanuni zinazotaja wenyeviti kuchaguliwa na
wajumbe wa kamati.
Hoja
nyingine ni kamati hiyo ya bajeti kulipwa posho ya Sh430,000 wakati
wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000 pamoja na kumteua
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba kuingia katika kamati hiyo ya
bajeti wakati mbunge huyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu.
Jana
Dk Kigwangalla aliwasilisha hoja yake kwa Katibu wa Bunge na kuongeza
madai mapya yakiwamo ya kuagiza kwa mabavu majedwali ya mabadiliko ya
sheria kwenda kwenye kamati ya bajeti, kuvunja masharti ya kanuni ya 48
inayotoa maelekezo ya namna ya kuwasilisha na kujadili jambo la dharura
na kutumia madaraka yake vibaya kwa kuvunja masharti ya Sheria ya The
National Assembly (Administration) Act (Cap.115) ya mwaka 2008.
Makinda
akijibu hoja hizo jana alisema alifanya uteuzi wa Chenge kuongoza
Kamati ya Bajeti kwa sababu kamati hiyo ni mpya na haikuwapo katika
kamati za awali, hivyo ni wazo ambalo lilitokana na mawazo ya Bunge la
sasa.
“Tulikuwa
tunafikiria jinsi Bunge linavyoweza kuisadia Serikali ipate vyanzo
vipya vya mapato. Kwa hiyo tumehitimisha wazo hili kwa kuamua kuwa na
Kamati ya Bajeti. Kamati hii haikuwapo na wala utaratibu wake wa
kikanuni haukuwapo. Niliamua na kanuni zinanipa uwezo huo kwamba niteue
mtu ambaye ninaamini anaweza kuisimamia katika hatua za mwanzo ili tuone
uzoefu utatufikisha wapi,” alisema Makinda na kuongeza:
“Kamati
hii hata Serikali ilikuwa haikubaliani na sisi, lakini katika muda
mfupi wa utendaji wake umefanya kazi kubwa na kama tusingekuwa na Mzee
Chenge ambaye ni mzoefu na anafahamu vizuri utendaji wa Serikali basi
tungeshindwa na mimi siko tayari kuanzisha kitu halafu nikashindwa”.
Kuhusu
posho, Spika aliungana na kauli ya Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashililah kwamba si wakati wote Kamati ya Bajeti imekuwa ikipewa malipo
zaidi, bali ni pale tu wanapofanya kazi nje ya siku na saa za kazi tena
kwa kibali chake.
“Lazima
walete maombi na waeleze kwa nini wanapaswa kufanya kazi kwa muda wa
ziada au siku za mapumziko na mimi nikisharidhia basi wanalipwa mara
mbili ya viwango vya kawaida na hiyo ni kwa mujibu wa taratibu na Kanuni
zetu,” alisema.
CHANZO
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment