Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013 ambayo
ilipitishwa na Bunge katika mkutano uliopita, ilikuwa na kasoro nyingi
ambazo zingekwaza kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Kutokana na hali hiyo, Spika Makinda ameliambia
Mwananchi kuwa kulikuwa na ulazima wa kufanya marekebisho katika sheria
hiyo hata kama Rais Jakaya Kikwete asingekutana na vyama vya siasa na
kukubaliana kuleta marekebisho katika kikao cha Bunge kinachoendelea
hivi sasa.
Licha ya Makinda kutokuwa tayari kuweka wazi
kasoro hizo, gazeti hili limebaini kuwa mambo hayo hayatofautiani sana
na yale yaliyobebwa kama ajenda na vyama vya upinzani vilipokutana na
Rais Kikwete, hivyo kuwezesha kuanza mchakato wa sheria hiyo kupitiwa
upya.
“Labda nikwambie hivi katika muswada ule
uliopitishwa siwezi kusema kilitokea nini, lakini kimsingi kuna
administrative issues (masuala ya kiutawala) nyingi ambazo kama sheria
ikibaki ilivyo, hata Bunge la Katiba haliwezi siyo tu kufanya kazi, bali
hata kuitishwa,”alisema Makinda.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Ofisi ya
Bunge tayari imewasilisha mapendekezo yake Serikalini ikiainisha maeneo
yapatayo kumi yenye kasoro zinazopaswa kufanyiwa kazi.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alikiri
kwamba ofisi yake imewasilisha mapendekezo yake Serikalini, lakini kama
ilivyokuwa kwa Makinda hakuwa tayari kuingia undani wa mapendekezo hayo.
Juzi Serikali ilikuwa ikifanya majadiliano ya
mwisho na wawakilishi wa vyama vyenye wabunge kuhusu marekebisho
yanayopaswa kufanywa katika sheria hiyo, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema muswada
huo ungewasilishwa jana kwa Katibu wa Bunge.
Dk Kashililah alisema walibaini upungufu kwenye
sheria hiyo baada ya muswada kupitishwa na Bunge Uchunguzi wa Mwananchi
umebaini kuwa Ofisi ya Bunge imefanya uchambuzi wa kina kuhusu umuhimu
wa kuendelea kuwapo kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tofauti na uamuzi
wa awali wa kuvunjwa kwa tume hiyo.
CHANZO;MWANANCHI
CHANZO;MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment