Home » » Wafugaji wataka ng’ombe wao

Wafugaji wataka ng’ombe wao



CHAMA cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kimetoa siku 14 kwa serikali kurejesha ng’ombe iliyowauza kwa mnada baada ya kuwakamata kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.
Akizungumza na Tanzania Daima, Mwenyekiti wa chama hicho, Ally Lumiye, alisema licha ya serikali kutangaza kusitisha operesheni ya kutokomeza ujangili na kuagiza ng’ombe wote waliokamatwa kabla ya baada ya operesheni hiyo warejeshwe kwa wafugaji bila faini, baadhi ya watendaji wamekaidi.
Alisema wanataka ng’ombe waliouzwa baada ya tamko la serikali warejeshwe kwa wafugaji katika kipindi cha siku 14 la sivyo watachukua hatua za kisheria ili haki za wahusika zipatikane.A
Lumiye aliongeza kuwa watendaji waliowauza ng’ombe na wanunuzi wanafahamika, hivyo ni vema wakarejesha mifugo hiyo kabla ya chama hicho kuchukua hatua za kisheria baada ya muda huo walioutoa.
Pia alisema chama chake kinamtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, awaombe radhi kwa kuwaita matapeli waliowachangisha sh 50,000 wafugaji ili waende Dodoma kuonana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
“Sisi si matapeli kama alivyotuita Waziri Lukuvi, ni kweli tuliwaambia wafugaji waje hapa Dodoma wakiwa na sh 50,000 lakini hazikuwa kwa ajili ya kuonana na waziri mkuu bali kugharimia mkutano mkuu tulioufanya siku chache zilizopita.
“Tunamtaka atuombe radhi la sivyo tutazunguka maeneo mbalimbali hapa nchini kuwaambia wanachama wetu kuwa nao ni matapeli kwakuwa wao ndiyo waliotuchagua na tunafanya kazi wanayotuagiza,” alisema.
Naye Katibu Msaidizi wa CCWT, Masanja Mtwale, alisema wanaamini Kamati Teule iliyoundwa na Bunge itasaidia kuibua na kutafutia ufumbuzi uovu unaofanywa na watendaji mbalimbali dhidi ya wafugaji.
Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi wa CCWT, Kusundwa Wamarwa, alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikiunda tume mbalimbali kuchunguza kadhia wanazozipata wafugaji lakini hazijatoa matunda mazuri kwa kuwa mtuhumiwa ndiye anayejichunguza.

CHANZO;TANZANIA DAIMA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa