Home »
» Mbunge ataka CDA ivunjwe
Mbunge ataka CDA ivunjwe
|
|
MBUNGE wa Dodoma Mjini, David Malole (CCM), amemuomba Rais
Jakaya Kikwete kuifumua Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa
madai kuwa ni chanzo cha migogoro ya ardhi katika Halmashauri ya
Dodoma.
Mbali na hilo, alisema kuwa yeye hawezi kuendelea kuwa mjumbe wa bodi
ya CDA ambayo kimsingi haijali haki za binadamu na inafanya kazi bila
kujali utu wa mtu ndiyo maana imekuwa ikibomoa nyumba za wananchi bila
majadiliano.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano katika viwanja vya Bunge mjini
hapa, Malole alisema ni bora kuifuta mamlaka hiyo na kutafuta njia
mbadala kuliko kuendelea kuwatesa wananchi wasiokuwa na hatia.
Mbunge huyo pia alihoji ni wapi viongozi wa mamlaka hiyo wanapata
jeuri ya kuwanyanyasa wananchi kwa kuwabomolea nyumba zao kwa madai
kuwa watu hao ni wavamizi.
“CDA imekuwa mwiba kwa wakazi wa Halmashauri ya Dodoma kwani wananchi
wengi kwa sasa wanaishi kwa shaka na wengine hawawezi kujenga nyumba
bora kutokana na hofu ya kubomolewa nyumba zao.
“Kibaya zaidi viwanja vinavyouzwa na CDA vinauzwa kwa bei ya juu
ambapo wananchi hawawezi kununua kwa wepesi na hiyo kama haitoshi
inakuwaje mtu anajenga mpaka anamaliza anaanza kuishi, leo unamwambia
ni mvamizi? Ina maana kitengo cha ukaguzi wa mazingira hakipo na kama
kipo wanalipwa mshahara wa nini?” alihoji Malole.
Mbunge huyo alitolea mfano wa wakazi wa Kikuyu ambao walilazimika
kurudisha kadi za CCM kwa madai kuwa serikali haiwajali na ndiyo maana
inabomoa nyumba zao licha ya kuwa na sera ya maisha bora kwa kila
Mtanzania.
Akijibu tuhuma hizo, Kaimu Mkurugenzi wa CDA, Paskasi Mulagili,
alisema kwa mujibu wa kanuni na taratibu na sheria, CDA inajipanga
kubomoa maeneo yote ambayo yamejengwa kiholela na kuvamiwa kinyume na
taratibu.
Akizungumzia suala la mbunge kujiondoa kwenye bodi kwa madai kuwa CDA
ni chanzo cha migogoro, alimtaka kutoa hoja binafsi bungeni kwa ajili
ya kulishawishi Bunge kuvunja CDA na si vinginevyo.
chanzo;tanzania daima
|
|
0 comments:
Post a Comment