Serikali imeendelea kushikilia msimamo wake wa
kutaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba ivunjwe mara baada ya kukamilisha
rasimu ya pili ya Katiba Mpya na kuikabidhi kwa Bunge Maalumu kwa ajili
ya kujadiliwa, Mwananchi limebaini.
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili zinasema,
suala la ukomo wa tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mstaafu Joseph Warioba
ndilo lililochukua sehemu kubwa ya mjadala katika vikao vya majadiliano
baina ya Serikali na vyama vyenye wabunge vinavyokutanishwa na Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD).
Majadiliano baina ya pande hizo yalihusu
marekebisho yanayopaswa kufanywa katika Sheria ya Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba 2013, ambayo ilipitishwa na Bunge katika mkutano
wake wa 12 baada ya kuwapo kwa malalamiko kwamba ina kasoro nyingi
ambazo zingekwaza upatikanaji wa Katiba bora.
Msimamo huo wa Serikali pia ni kama kupuuza maoni
ya Ofisi ya Bunge ikiongozwa na Spika, Anne Makinda ambayo iliwasilisha
maoni yake ikikosoa hatua ya kuwekwa kando kwa Tume ya Warioba kwa
maelezo kwamba kutokuwepo kwake kutaathiri utekelezaji wa vifungu
vingine vya sheria hiyo.
Jumapili iliyopita, Serikali ilifanya mashauriano
ya mwisho na wajumbe hao wa vyama katika kikao kilichofanyika Ofisi za
Bunge Dodoma, lakini habari zinasema hakukuwa na mwafaka juu ya ukomo wa
tume hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi akizungumza na gazeti hili jana
alisema Serikali tayari imewasilisha muswada huo katika Ofisi ya Katibu
wa Bunge, na kwamba mamlaka ya hatua zinazofuata yapo kwa Spika.
Kadhalika waziri huyo alikiri kuwapo kwa kikao cha
mashauriano kuhusu marekebisho ya sheria hiyo, lakini alikataa
kuzungumzia msimamo wa Serikali kuhusu suala la Tume ya Warioba.
“Sheria iliyopitishwa na Bunge, kisha kusainiwa na Rais inasimama hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.”
chanzo;mwananchi
chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment