Dodoma. Waziri Mkuu
Mizengo Pinda pamoja na mawaziri wake wawili; Khamisi Kagasheki
(Maliasili na Utalii) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo David
wameingia matatani kutokana na shinikizo linalowataka wang’oke katika
nafasi zao.
Pinda pamoja na mawaziri hao wanatakiwa kuachia ngazi kama hatua ya
kuwajibika kutokana na matukio ya vifo na baadhi ya watu kujeruhiwa,
katika matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja na
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili kwa upande mwingine.
Jana wabunge walicharuka na kuwataka mawaziri waliohusika katika
Operesheni Tokomeza Ujangili wawajibishwe wakieleza kutoridhishwa na
maelezo waliyoyatoa mapema jana, baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Kelele za wabunge zilizuka baada ya wabunge kuanza kuchangia maelezo ya
Serikali kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima, hifadhi za wawekezaji
na maelezo ya Serikali kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili.
Aliyekuwa wa kwanza kuchangia mjadala huo ni Mbunge wa Kilolo, Profesa
Peter Msola (CCM) ambaye katika hitimisho lake alitoa hoja ya kuundwa
kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kile ambacho alikiita kuwa ni
unyanyasaji wa wafugaji na uporaji wa mifugo yao.
Profesa Msola alielekeza shutuma zake kwa Serikali kuwa ilifanya
operesheni zake kwa pupa bila kufanya maandalizi hivyo kuwaathiri
wananchi wasiokuwa na hatia.
Spika wa Bunge, Anne Makinda kabla ya kuahirisha kikao cha Bunge jana
mchana aliridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kwa ajili ya
kuchunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji, wakati ‘madudu’ ya
Operesheni Tokomeza Majangili yatachunguzwa kupitia Kamati ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Chimbuko la hoja
Jana asubuhi kabla ya Bunge kuanza kikao chake, Spika Makinda alitoa
taarifa kwamba Kikao cha Kamati ya Uongozi kingekutana wakati kipindi
cha maswali na majibu kikiendelea, kwa lengo la kutoa mwelekeo wa
mjadala wa hoja za dharura.
Hoja hizo ni zile zilizotolewa na wabunge wawili kwa nyakati tofauti;
Alphaxard Kangi Lugora wa Mwibara (CCM) kuhusu Operesheni Tokomeza
Majangili na Saidi Nkumba wa Sikonge (CCM), kuhusu vita baina ya
wakulima na wafugaji.
Kamati hiyo ilikutana baada ya kipindi cha maswali na majibu na Spika
Makinda alitoa taarifa za kusitisha shughuli nyingine, ili wabunge
waweze kujadili masuala hayo ambako kabla ya kuanza mjadala aliwaita
mawaziri kutoa taarifa zao.
Alianza Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki ambaye katika
maelezo yake alihitimisha kwa kutangaza kusitisha Operesheni Tokomeza
ili kupitia mpango huo na kufanya maboresho ili kuondoa upungufu uliopo.
Licha ya kueleza sababu nyingi zilizofanya Serikali kuendesha operesheni
hiyo, alisema ina manufaa makubwa katika kuokoa wanyama aina ya tembo,
lakini waziri alihitimisha kwa kusema itakuwa ni busara kuifanyia
tathmini wakati ikiendelea, hivyo kutangaza kuisitisha mara moja.
Kwa upande wake Dk Mathayo alitoa maneno ya kuomba radhi na kuwapa pole
watu waliopatwa na usumbufu ikiwa ni pamoja na kupoteza mali zao na
mifugo.
Mathayo aliwaeleza wabunge kuwa Serikali imepanga kujenga malambo katika
maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji kupata maji ili
kupunguza safari za kuhamahama kutoka eneo moja kwenda jingine.
Shinikizo kwa Pinda
Baada ya kumaliza hotuba zao, wabunge kadhaa walipata nafasi ya
kuchangia maelezo hayo huku wengi wakielekeza shutuma zao kwa mawaziri
hao na wenzao wa Mambo ya Ndani ya Nchi na yule wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa.
Wabunge wawili wa Chadema, Paulina Gekul (Viti Maalumu) na John Shibuda
(Maswa Mashariki) walitaka Waziri Mkuu Pinda ajiuzulu kutokana kushindwa
kwake kudhibiti mauaji na mateso kwa wananchi.
Gekul alisema kinachotokea sasa ni utekelezaji wa kauli ya Pinda
aliyoitoa bungeni akisema wahalifu wapigwe tu pamoja na ile ya Kagasheki
aliyoitoa mjini Arusha akisema majangili watakaokamatwa wamalizwe
hukohuko kwenye hifadhi.
Mbunge huyo alieleza operesheni hiyo kwamba imesababisha mauaji ya watu
wasio na hatia ikiwemo mama Emiliana ambaye alifuatwa akiuza nyanya,
lakini akateswa hadi kufa na hadi sasa mwili wake bado uko katika
Hospitali ya Babati baada ya wananchi kugoma kuuzika.
Shibuda kwa upande wake alisema Pinda anapaswa kufungua milango kwa
mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu haraka, kutokana na kulea uzembe ambao
umesababisha madhara makubwa kwa wafugaji.
Shibuda alisema kuwa Wizara ya Mifugo imekuwa na mtazamo hasi lakini
akasisitiza kuwa uzembe wa viongozi wa ngazi za mikoa, wilaya hadi
vijiji unatokana na ukimya wa Pinda ambaye anashindwa kuchukua hatua
yoyote dhidi yao.
Wabunge wengine
Kwa upande wake Nkumba aliunga mkono kuundwa kwa kamati teule, lakini
akasisitiza kuwa mawaziri hao wanne wana hoja za kujibu ndani ya chama
tawala CCM na kwa Rais, vinginevyo Serikali haipaswi kuendeshwa na
viongozi wazembe wa aina hiyo.
“Mawaziri mnaosimamia jambo hilo mnayo hoja ya kujibu kwa chama chenu
tena bahati nzuri wote mnatoka CCM, ambao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ninyi wa Mifugo na
Uvuvi pamoja na Maliasili na Utalii, nasema hatuko pamoja na watu
wazembe hata siku moja,” alisema Nkumba.
Mbunge huyo alionya kuwa umefika wakati ambao Serikali inatakiwa iache
tabia ya kuwadanganya wabunge kuwa itapeleka taarifa bungeni, lakini
mambo yakishapoa basi inakaa kimya na akataka maelezo ya kina majangili
wakubwa wako wapi, na kwa nini wasikamatwe na badala yake kinachofanyika
ni kuendelea kuwatesa wasiokuwa na hatia, kisha akashawishi wabunge
wote wazikatae taarifa za mawaziri hao.
Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alizikataa taarifa za mawaziri wote
wawili kwa madai ya kupikwa na kujaa giliba za kuwahadaa wananchi.
“Mawaziri hawa wataponea wapi katika mkono huu, watu wamekufa,
wameteswa, mifugo imeporwa na mingine kupigwa risasi wao wapo tu, nasema
wataponea wapi ikiwa ushahidi wote uko hapa,” alisema Lugola na
kuongeza:
“Mawaziri hawa wataponea wapi kama damu ya Dasu Lutaligula (Kilombero),
Madirisha Luchagula (Mulele), Baya Tambi (Ulanga) wafugaji watano
waliokufa huko (Mtimbira- Ulanga ), vilema vya kudumu Luhende, Ofisa
Tarafa (Mpimwe) Diwani wa Maji Moto, wafugaji watano wa Mtimbira
waliopata vilema kutokana na waliyotendewa na Serikali ya Chama Cha
Mapinduzi, hivi wataponea wapi kwa damu za hao?”
Alisema zaidi ya ng’ombe 500 walipigwa risasi katika mpango wa mradi wa
watu wachache wa kutaka kujinufaisha wenyewe ama kwa kushirikiana na
viongozi wa juu.
Aliwatuhumu askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), polisi na
askari wa wanyamapori, kuwa wamekuwa wakiua watu ovyo na wengine
kubakwa, lakini Serikali inawakingia kifua hali inayoonyesha kuwa kuna
udhaifu ndani ya Serikali.
Katika michango yao, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM) alisema
maelezo yaliyowasilishwa na mawaziri ni mzaha, huku akiwaonya mawaziri
kuacha tabia ya kupuuza hoja za wabunge, kwani wanapozungumza huwa
tayari wamefanya utafiti.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF) na Mbunge wa
Kuteuliwa James Mbatia (NCCR-Mageuzi), walisema yote yametokea kutokana
na uzembe wa viongozi ikiwemo mawaziri kushindwa kutimiza wajibu wao.
Hadidu za rejea
Jana jioni Spika wa Bunge, Anne Makinda alimpa nafasi Profesa Msola, ili
aelezee malengo ya kamati teule itakayoundwa ambapo alisema itakuwa na
jukumu la kuchunguza na kuchambua sera mbalimbali zinazohusu ardhi,
kilimo, mifugo, maji, wanyamapori na uwekezaji ili kubaini kasoro za
ardhi, hatimaye kuleta mapendekezo bungeni yatakayoondoa migogoro ya
ardhi inayoendelea kati ya wakulima, wafugaji, hifadhi, uwekezaji na
watumiaji wengine wa ardhi.
Alizitaja hadidu za rejea za kamati teule kuwa ni kuchambua sera
mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi kubainisha kasoro zilizopo
katika sera hizo, kuchunguza mikakati iliyowekwa na Serikali, kuchambua
mikakati yote ya Serikali ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na
wafugaji
Nyingine ni kuchambua mikakati ya kulinda vyanzo vya maji, uharibifu wa
mazingira na kutoa mapendekezo yatakayoondoa migogoro yote kudumisha
uhusiano mzuri na utengamano na mambo mengine ambayo kamati itaona
yanafaa.
Akiboresha hadidu za rejea Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema),
alisema ni vyema kamati teule hiyo ikapitia ripoti mbalimbali tume na
kamati zilizoundwa kuchunguza suala ya matumizi ya ardhi ikiwemo ya
Profesa Shivji.
Alisema kuwa kumekuwa na kawaida ya kuunda tume ambazo zimekuwa ni siri na utekelezaji wake hakuna.
Mnyika alisema kuwa ni vyema katika kuongeza hadidu za rejea ya kushughulikia uwajibikaji pale ambapo kuna kasoro za utendaji.
Mbunge wa Tunduru Abdallah Mtutura (CCM), alisema wapo watu ambao
wameuawa kwa kisingizio kuwa ni majangili huku wengine wakijificha
maporini kuogopa operesheni hiyo.
Aliunga mkono kuongezwa kwa hadidu ya kuchunguza mauaji na watu walioteswa katika operesheni hiyo.
Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama (CCM), alitaka kuwepo kwa muda
maalumu wa kamati teule kufanya kazi kwa kuwa jambo hilo ni zito.
Alisema kumekuwa na tume nyingi ambazo hazijaonyesha matokeo yake na
kutaka kamati hiyo itakayoundwa iwe ya mwisho katika utekelezaji.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Mosses Machali (NCCR- Mageuzi), alisema
operesheni hiyo imefanya zaidi ya ugaidi na unyama na kuomba waliohusika
na mauaji na utesaji wa watu kupimwa akili.
Kwa upande wake Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed Mnyaa, (CUF),
alitaka kuwepo kwa fidia kwa watu walioathirika na operesheni hiyo.
Akihitimisha hoja hiyo, Profesa Msola alisema mapendekezo yote
yataingizwa katika hadidu za rejea ili yasaidie katika utendaji wa
kamati hiyo teule.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema majina ya wabunge watakaounda kamati hiyo, yatatajwa Jumatatu ijayo.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment