Home » » OUT Dodoma yahitaji Mkongo wa Taifa

OUT Dodoma yahitaji Mkongo wa Taifa

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Mkoa wa Dodoma kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kutokuunganishwa na Mkongo wa Taifa na kusababisha kukosekana kwa mawasiliano muhimu.
Kutosekana kwa Mkongo Taifa chuoni hapo  kunasababisha wanafunzi wa chuo kukosa kutumia teknolojia muhimu na kusababisha maendeleo ya chuo kuwa chini.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi OUT Mkoa wa Dodoma, Maulid Maulid alipozungumza katika sherehe za kuwapongeza wahitimu 155 wa chuo hicho mkoa wa Dodoma.
Alisema kuwa licha ya kuwa mafanikio ya kupata wanafunzi wengi ambao wanajiunga na chuo hicho, lakini kwa sasa wanakumbana na changamoto mbalimbali ambazo zinasababisha kuwepo kwa utendaji kazi ambao haufikii viwango.
Alisema chuo hicho kinatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kulinda heshima ya kituo hicho ukilinganisha na vituo vingine.
Maulidi alizitaja changamoto zinazokikabili chuo hicho katika mkoa wa Dodoma ni ufinyu wa bajeti, jambo ambalo linasababisha kushindwa kuwa na gari la kituo na kutokuweza kusafiri na kuwafikia wanafunzi pale inapotakiwa kufanya hivyo.
Alisema changamoto nyingine ni ukosefu wa ukumbi wa kufanyia mitihani na kukosekana kwa ardhi kwa ajili ya kujiandaa na ujenzi wa majengo ya chuo hicho katika miaka michache ijayo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Alfred Msovella, alisema kwa sasa Watanzania wanatakiwa kusaka elimu kwa nguvu nyingi vinginevyo wataonekana mzigo katika taifa.
“Nataka kuwaeleza kuwa kwa sasa ulimwengu tulionao si wakati wa kusoma kwa kuangalia ukubwa wa majengo kama ilivyo UDOM ama vyuo vingine vikuu kinachotakiwa ni kuangalia ni jinsi gani mtu anavyoweza kupata elimu kwa njia ya mtandao na kuweza kufikia lengo lake,” alisema.
“Kuna watu wengi wamepata elimu bila hata kuingia darasani lakini walihakikisha wanafanya masomo yao kwa njia ya mtandao na wameweza kufanya vizuri,” alisisitiza Msovella.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa